Habari za Punde

Wadau wa Vitendo Vya Udhalilishaji Pemba Waungana Pamoja Kujadilim Mbinu Mpya za Kukabiliana na Vitendo hivyo.

Naibu mrajisi wa Mahakama kuu Pemba, Abdul Razak Ali akizungumzia suala la mashahidi kushindwa kulipwa nauli zao wanapofika mahakamani
Hakimu wa Mahakama ya Mkoa Wete, Abdalla Yahya Shamhun akizungumza .
Mratibu  wa Dawati la kijinsia na mkuu wa upelelezi Jeshi la Polisi Wete, ASP Fakih Yussuf akizungumza wakati wa mkutano.

WADAU wa kupambana na vitendo ya udhalilishaji kisiwani Pemba wameungana pamoja kujadili mbinu mpya za kukabiliana na vitendo hivyo katika jamii ambavyo vinaonekana kuwa ni tishio siku hadi siku visiwani hapa.

Wakizungumza katika mkutano wa mtandao wa kupiga uhalilishaji Pemba ulioandaliwa na Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ) na kuwashirikisha mahakimu wa mahakama kuu Pemba, maafisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP), Dawati pamoja na maafisa ustawi wa jamii walisema  ipo haja kwa kila mmoja na taasisi husika kushilikiana katika kufuatilia kesi  kwa ukaribu ili zipatiwe hukumu kwa wakati.

Hakimu wa Mahakama ya Mkoa Wete, Abdalla Yahya Shamhun, alisema iwapo jamii itakubali kubadilika na kuripoti matukio kwa wakati na wahusika wengine kuwajibika ipasavyo itakuwa ni mwanzo wa kukomesha kutokea kwa matukio hayo.

“Jamii ikiripoti matukio kwa wakati na wahusika wengine wafanye wajibu wao hapa ndipo tutakapo fika sehemu ambayo tunataka tufike katika masuala haya” alisema.

Aidha hakimu huyo alikiri kuwepo kasoro kwa baadhi ya watendaji na wasimamizi wa kesi hizo ndani ya mahakama na kusisitiza zaidi iwapo vyombo vyote vitasimama imara itasaidia kuziba mianya kwa baadhi ya mahakimu wanaotaka kuharibu kesi kwa maslahi yao wenmyewe.

Alisema, “sisi tunakiri kwamba mahakama tunayo matatizo kwa sababu mahakimu tumetofautiana, lakini kama huko chini kutatengenezwa vizuri, Dakatari, Polisi akapeleleza kwa wakati, mashahidi wakatoa ushahidi wao vizuri kukawa na mtiririko mzuri wa ushahidi hakuna hakimu yeyote anayeweza kuharibu kesi hiyo.”

Katika hatua nyingine hakimu huyo ameitaja Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba kuwa ndiyo inaongoza kwa kesi zake kufutwa kutokana na mashahidi kugoma kwenda kutoa ushahidi mahakamani.

“Hakuna sehemu ambayo kesi nyingi zinakufa kama Wilaya ya Micheweni. Imefika wakati mahakama tunatoa waraka ili mashahidi wakamatwe kuletwa mahakamani lakini hawakamatwi. Zipo kesi nyingi tunatarajia kuzifuta kwasababu hakuna mashahidi waliokuja mahakamani ili tuendelee na kesi hizo” alisema.

Naibu mrajisi wa Mahakama kuu Pemba, Abdul Razak Ali akizungumzia suala la mashahidi kushindwa kulipwa nauli zao wanapofika mahakamani kutoa ushahidi kwa mjibu wa sheria alisema tatizo hilo linatokana na mahakama kutopata pesa hizo kwa wakati jambo ambalo pia ni tatizo kwa upande wao.

Alisema, “tatizo la mashahidi kutopewa pesa zao wanapofika mahaamani kutoa ushahidi linatokana na Mahakama kutopokea pesa hizo kwa wakati ili kuwezesha mashahidi kufika mahakamani hili kweli ni tatizo bado kwa upande wetu.”

Nae mratibu wa Dawati la kijinsia na mkuu wa upelelezi Jeshi la Polisi Wete, ASP Fakih Yussuf alisema maafisa Polisi wanaoshuhulikia kesi hizo wanakabiliana na changamoto ya ukosefu wa bajeti ya kuwezesha kufuatilia matukio hayo jambo linalopelekea kushindwa kuchukua hatua kwa wakati.

“Sisi Jeshi la Polisi tuna hali mbaya sana na tunapata taabu zaidi katika kufuatilia masuala ya udhalilishaji. Unaweza kupata taarifa kwa wakati lakini unashindwa kuchukua hatua kwa wakati kutokana na kukosa uwezeshaji. Robo ya mishara yetu inakwenda kwa kushughulikia kazi za Polisi na huo ndio ukweli wenyewe,” alisema.

Aidha ASP Fakih aliitaka jamii kujenga utaratibu wa kuchukua hatua mapema kwa kuwakamata watuhumiwa ili kuepusha tatizo la watuhumiwa kukimbia wanapotekeleza matukio hayo.

“Jamii isisubiri mpaka Polisi waje ndipo wamkamate mtuhumiwa na badala yake wanatakiwa kuchukua hatua za kumkamata mtuhumiwa huyo mara moja tukio linapotokea ili asiweze kukimbia.”

Mapema Salma Abdalla Hemed ambaye ni mwanamtandao wa kupinga udhalilishaji alisema kesi kuchukua muda mrefu na kufutwa ni moja ya changamoto zinazowakatisha tamaa wananchi kuendelea kutoa mashirikiano ya kufuatilia kesi hizo.

Alisema, “tunaibua kesi nyingi sana lakini kesi nyingi hazifiki sehemu nzuri na watuhumiwa tunawaona wameachiwa huru. hii inawakatisha tamaa kwani wanahisi sisi tunaowahamasisha kuzifuatilia kesi hizi ndio tunawadhalilisha watoto wao na  linapotokea tukio la udhalilishaji tukimfuata mzazi wanatuona kama maadui na tunawahangaisha tu hakuna haki yoyote.”

Rashid Hassa Mshamata, aliliomba Jeshi la Polisi kuongeza ufuatiliaji wa watuhumiwa wanaotoroka baada ya kutekeleza matukio hayo jambo linalopelekea kesi nyingi kushindwa kuhukumiwa kwa sababu ya mtuhumiwa kutoroka.

“Ukiibua kesi ukaambiwa mtuhumiwa kakimbia hiyo kesi imekwisha. Tunaambiwa serikali ina mkono mrefu lakini kwa Pemba ikishatokezea hivo watuhumiwa hawafuatiliwi jambo ambalo linapelekea kesi nyingi zinazofutwa mahakamani sababu zake ni mtuhumiwa kukimbia. Hili ni tatizo kwetu.”

Kwa upande wake mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said alisema wadau wa kupambana na udhlilishaji wapaswa kushirikiana kwa pamoja kila mmoja kwa nafasi yake ili  matendo hayo yaweze kumaliza  Zanzibar.

Nae Ali Mohamed Abdalla, meneja programu kutoka TAMWA Zanzibar alisema mkutano huo umekuwa ni chachu ya kuchochea nguvu zaidi kwa wadau hao kupambana na vitendo hivyo.

“Kupitia jukwaa hili tumeweza kujua wapi kasoro zilipo katika kupambana na janga hili kwenye jamii yetu na tunaamini kupitia hapa wadau kila mmoja atakwenda kufanya kazi kwa mashirikiano ili lengo letu la kumaliza udhalilishaji Zanzibar liwez kufanikiwa,” alisema.

Mkutano huo ulioandaliwa na TAMWA Zanzibar uliolenga kuwawezesha wana mtandao kufanya ufuatiliaji wa kesi na kujadili changamoto zinazowakwaza ni utekelezaji wa mradi wa kutumia jukwaa la Habari kumaliza udhalilishaji Zanzibar unaotekelezwa kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Denmark (DANIDA) ni mwendelezo wa juhudi za kupambana na vitendo hivyo tishio Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.