Habari za Punde

Serikali Kuendelea Kudhibiti Mfumko wa Bei Nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akijibu swali la Mhe. Cecilia Daniel Paresso (Viti Maalum),Bungeni jijini Dodoma. 

Na. Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali imeeleza kuwa itaimarisha usimamizi wa sera ya fedha na bajeti ili mfumuko wa bei uendelee kubaki ndani ya wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la MheCecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum aliyehoji mkakati wa Serikali wa kudhibiti mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa ulioanza tangu Desemba, 2020 ambao umefanya gharama za maisha kupanda.

Mhe. Nchemba alisema kuwa mikakati ya Serikali ni kuimarisha usambazaji wa chakula kutoka maeneo ya uzalishaji hadi katika maeneo ya walaji pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi katika masoko.

Mfumuko wa bei ulipanda kutoka asimilia 3.2 mwezi Desemba 2020 hadi asilimia 3.5 mwezi Januari 2021 kutokana na upungufu wa baadhi ya bidhaa sokoni ambao hutokea mara kadhaa katika vipindi vya mwanzoni mwa mwaka”, alisema Dkt. Nchemba.

Alifafanua kuwa mfumuko wa bei ulishuka kufikia asilimia 3.3 mwezi Februari 2021 ikiashiria kuwa bidhaa na huduma zilianza kupatikana kwa bei nafuu kulinganisha na mwezi Januari 2021.

Kuhusu bei ya bidhaa za sukari na mafuta ya kupikia kuwa juu Mhe. Nchemba alisema kuwa kwa takribani miaka zaidi ya 10 Serikali imefanikiwa kushusha mfumuko wa bei na kufikia kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0 ambacho ni kiwango cha Afrika Mashariki.

“Serikali imejikita kwenye kuongeza uzalishaji wa sukari ambapo kutakuwa na upanuzi wa mashamba pamoja na uzalishaji wa sukari ambao utaenda kutoa jibu la uhakika na la kudumu kuhusu bei ya bidhaa hiyo”, alisema Waziri Nchemba.

Aliongeza kuwa changamoto ya bei ya sukari ilitokea baada ya kupungua kwa uzalishaji wa ndani na hivyo kuagizwa kutoka nje, hivyo uzalishaji wa ndani utatoa jibu la kudumu la mabadiliko ya bei ya sukari.

Mhe. Nchemba alisema kuwa juhudi za Serikali zinaendelea katika kuhamasisha kilimo cha mazao yanayotumika kuzalisha mafuta ili kupata jawabu la kudumu la upungufu wa mafuta unaosababisha kupanda kwa bei.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.