Habari za Punde

ACT Wazalendo yamtambulisha mgombea wake jimbo la Konde

Kaimu Mwenyekiti wa ACT wazalendo  Dorothy Semu akipokea kadi za wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo waliokihama chama hicho kwa niaba ya wafuasi 28 kutoka kwa Katibu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wa chama hicho Shafi Muhammed Shafii.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha ACT wazalendo Dorothy Semu akimtambulisha kwa wananchi  Mgombea Ubunge wa Jimbo la Konde kupitia chama hicho Muhamed Said Issa katika mkutano wa hadhara wa ufunguzi wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Konde Polisi. 

Na Talib Ussi

Kaimu Mwenyekiti wa chama cha Act Wazalendo Dorothy Semu amewataka wanachi wa Jimbo la konde Kumchaguwa Mgombea Ubunge Jimbo hilo kupitia Chama hicho  Muhammed Said Issa ili awaondolee kero zinazowakabili ikiwemo miuondombinu na Ajira.

Kaimu huyo aliyaeleza Jimboni humo katika viwanja vya Konde Polisi Wilaya ya Micheweni Mkoa kaskazini Pemba katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni wa kumnadi mgombea wa chama chao katika  uchaguzi mdogo wa Ubunge kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Khatib Said Haji.

Alisema kuwa anaelewa shida walizonazo juu ya uwepo barabara mbovu na ukosefu wa ajira kama watamchagua Mgombea wa ACT Wazalendo Muhammed Said Issa anauhakika matatizo hayo yataondoka.

Alieleza kuwa Mgombea huyo yuko tayari kuazisha vikundi vya ushirika vya aina mbali mbali ili wapiga kura wake waweze kujiajiri kwa madhumuni ya  kujikwamua kimaisha.

Alisema Mbunge aliyepita ambaye alitokana na chama hicho alifariki mwanzoni mwa mwaka huu Khatib Said Haji alifanya maendeleo Makubwa.

“Ili pale alipopabakisha marehemu Khatib na kumuezi juhudi zake nakuombeni wananchi wa Konde twendeni tarehe 18 mwezi huu tukamchague Muhamed Said Issa wa ACT wazalendo kwa kura nyingi” alieleza Dorothy.

Sambamba na hilo Mama Dorothy aliiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki katika uchaguzi huo ili wananchi wa konde wachague Mbunge wanayemtaka.

Alieleza uzoefu walionao  uchaguzi Mkuu uliopita alidai wagombea wengi waliotangazwa hawakuwa washindi halali.

“Tunaiyomba NEC kutenda haki vyenginevyo tusijetukatafuta mchawi, tunajua Jimbo hili ni la kwetu wala halinashaka, wakitufanyia vurugu hatutakuwa tayari na sisi kuvumilia” alisema Dorothy.

Kwa upande wa uwepo wa mikutano ya hadhara Nchini Mama Dorothy alimuomba Rais wa Jamuhui ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuheshimu matakwa ya katiba inayotaka uwepo uhuru wa Vyama vya siasa kuendeleza shuhuli zao ikiwemo mikutano ya hadhara bila vikwanzo vyovyote vile.

“Unapozuia mikutano ya hadhara ni sawa wewe Rais wetu unavunja katiba na kujifanya kuwa juu ya katiba kitu ambacho hakikubaliki katika ulimwengu huu Demokrasia” alisema Dorothy.

Alisema vyama siasa vinatakiwa viongeze wanachama kila siku ili kuwa na nguvu na vinapozuiwa kufanya mikutano ni sawa na kunyimwa kazi hiyo.

“Vyama vya siasa kazi yake ni siasa sasa leo kwa sababu tuu unaogopa kuondolewa madarakani unawazuiya kazi zao, tunakuomba usivunje katiba” alisema Dorothy.

Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho na wananchi kwa wingi ulionekana kuibua hamasa upya katika kuendeleza demokrasia nchini

Mapema akimkaribisha Kaimu huyo Makamu mwenyekiti wa chama hicho Juma Duni Haji alisema vyombo vya ulinzi vimekuwa na tabia ya  kuingilia chaguzi nyingi kwa kuwatesa wapinzani jambo alilodai halikubaliki kisheria.

“Watu wote ni sawa kwenye sheria lakini vyombo vya ulinzi hasa vikosi vya SMZ husababisha fujo na kuwateka baadhi wanachama wa vyama vya Upinzani na kuwatesa sana” alisema Duni.

Alisema Chama chao kimeingia kwenye maridhiano ili kusahau yale yalikuwa yanatokea katika chaguzi zilizopita kwa lengo kuwaunganisha wananchi kuwa kitu kimoja.

“Hii nchi sio ya CCM pekeyao ni ya wazanzibar wote kwa maana hiyo watu wote ni sawa, tufanyeni chaguzi ambazo tutawapatia wananchi nafasi ya kuchagua kiongozi wanayemtaka” alisema Duni.

Aliwaomba Marais wa Tanzania na Zanzibar kuzuia viashiria vyovyote vile ambavyo vitapelekea kuharibu umoja ambao umeasisiwa na viongozi waliotangulia.

Alisema sasaivi wananchi wanafanya kazi kwa pamoja kwa hiyo hakuna haja ya kuleta vurugu ambayo inaweza kuwarejesha kwenye mfarakano jambo alilieleza sio kitu chema kwa sasa.

Kufuatia kauli hiyo,  Duni aliwaomba wanachi wa konde kujitokeza kwa wingi kumchagua mgombea wa Act wazalendo Muhammed Said Issa.

Kwa upande wake Mgombea Ubunge wa chama hicho Muhammed Said Issa aliwataka wananchi wa Jimbo hilo kuwa na imani juu yake na kwennda kumchagua kwa kura nyingi muda utakapofika.

“Nichagueni kwa kura nyinyi na mimi nakuhakikishieni stowaunguasha, nitashirikiana na nyinyi ili kero zoote tulizonazo tuweze kuziondowa kwa uwezo wake Allah” alisema Issa.

Alisema endapo wananchi wa Jimbo hilo watampeleka Bungeni atahakikisha anaazisha vikundi vya ushirika vya aina mbai mbali vikimo vya wakulima, wafugaji na wavuvi.

“Nitakapofanya hivyo itakuwa rahisi kwangu mimi kuongeza nguvu na kuwatafutia mikopo ya kuendeleza miradi hiyo” alisema Mgombea huyo.

Aliwataka wapiga kura wa Konde wote kushikamana kwa pamoja na kumchagua yeye kwa kura nyingi ili mara nyengine wapinzani wao washindwe kujitokeza kwenye chaguzi nyengine.

“Khatib alikuwa kaka yangu na alikuwa rafiki, lakini kubwa alikuwa mtetezi wa wanyonge na mwenye kupigania  maendeleo ya wazanzibar pamoja na sisi watu wa kondo,  nikotayari kuyaendeleza kwa uwezo wake Allah” alisema

Uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la konde utafanyika tarehe 18 mwezi huu kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Marehemu Khatib Said Haji.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.