Habari za Punde

Alhaj Dk. Mwinyi Amewataka Waislam Nchini Kuendelea Kumuomba Mwenyenzi Mungu Kudumisha Amani Iliopo Nchini.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid Munawar Chumbuni Wilaya ya Mjini Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka waislamu nchini kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu adumishe amani iliopo ili Taifa liweze kupata maendeleo yanayohitajika. 

Alhaj Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo katika salamu zake kwa waislamu baada ya kukamilisha Ibada ya Sala ya Ijumaa, iliofanyika Masjid Munnawar uliopo Polisi Chumbuni , Wilaya ya Mjini Unguja.

Amesema ili Taifa liweze kupata maendeleo yanayohitajika, waislamu wana wajibu wa kumuomba Mwenyezi Mungu, alijaalie kila la heri na kudumisha amani iliopo.

Aidha, amewataka waislamu kuiombea dua nchi pamoja na Viongozi wake ili waweze kufanikisha  dhamira ya kuliletea Taifa maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi amekubali ombi la waumini wa mskiti huo la kusaidia upatikanaji wa Mazulia mapya kwa ajili ya kuswalia.

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, aliwasisitiza waislamu kuzingatia sifa na taratibu za kisheria katika kuchinja wanyama  kuelekea Idd el Adh-ha kwa kuwa jambo hilo ni la Ibada.

Aliwataka waislamu  kuepuka kuchinja wanyama wenye ila au wenye athari  na akatumia fursa hiyo kuelezea  umuhimu wa kuchinja wanyama wenye sifa (vigezo) na afya njema.

“Kuchinja ni wajibu wa kila muislamu mwenye uwezo, hii ni amri ya Mwenyezi Mungu”, alisema.

Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Simai Juma Ali aliwaeleza waislamu Ubora wa siku kumi (10) za mwezi wa Mfungo tatu pamoja na fadhila zake na kuwataka kuongeza juhudi kumcha Mwenyezi Mungu, kwa kuzidisha ibada ya Sala za Sunna, kusoma sana Qoraan, pamoja na kuwaombea dua wazazi, viongozi na Taifa kwa ujumla.

Sheikh Khalid alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waislamu wajibu walionao katika kuchinja kwa  mujibu wa muongozo wa Dini ya Kiislamu.

Aidha, akasisitiza  haja ya waislamu kushiriki Ibada ya sala ya Idd el Hajj kwa mujibu wa utaratibu.

Wakati huo huo, Alhad Dk.Mwinyi alifika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja kuwajuulia hali wagonjwa waliolazwa Hospitalini hapo, ikiwa ni utamaduni wake aliojiwekea.

Miongoni mwa wagonjwa hao ni pamoja na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto Mhe.Nassor Ahmed  Mazrui pamoja na wagonjwa wengine wanaosumbuliwa na maradhi mbali mbali.     

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.