Na Mwashungi Tahir Maelezo 9-7-2021
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu amewataka mahakimu kufanya kazi zao kwa uadilifu ili waweze kuondokana na malalamiko katika sehemu zao za kazi wanazotarajiwa kuzifanya kila siku.
Hayo ameyasema huko katika ukumbi wa Vuga wakati alipokuwa akiwaapisha Mahakimu Haroub Amour Bakari na Hidaya Muhamed Mussa kuwa wasuluhishi na waamuzi katika kitengo cha usuluhishi wa migogoro ya kazi kilicho chini ya kamisheni ya kazi.
Amesema kiapo hicho kimefanywa chini ya kanuni ya kumi na moja no(5) ya usuluhishi na uwamuzi wa kanuni za mwaka elfu mbili na kumi na moja 2011.
Aidha amesema kutokana na kuapishwa kwa wasuluhishi na waamuzi hao kutazidisha idadi ya wasuluhishi na waamuzi katika shughuli za kazi na kutarajia kwenda vizuri kazi hizo za kila siku.
Vile vile Jaji Omar amewataka mahakimu hao kuacha upendeleo katika sehemu zao za kazi na kujitahidi kutekeleza majukumu yanayowakabili na kuondosha malalamiko kwa wananchi kwa haraka ili waweze kuondokana na mrundikano wa malalamiko yanayohusu sehemu za kazi.
Hata hivyo amewasisitiza kufanya kazi kwa mashirikiano na kuwatakia mafanikio mazuri katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku na kuepuka kuweko na migogoro.
No comments:
Post a Comment