Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Aendelea na Ziara Yake Mkoa wa Kusini Wilaya ya Kati Unguja.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inatambua kuwepo kwa mgogoro wa ardhi unaowahusisha  wananchi wa shehiya ya Ubago dhidi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kambi ya Ubago.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo alipozungumza na wananchi wa shehiya za Ubago, Dunga na Binguni, mara baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Binguni, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake Mkoani humo, ambapo pamoja na mambo mengine alisikiliza changamoto mbali mbali za wananchi.

Amesema tayari Serikali imeunda Tume maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusiana na mgogoro huo, na kusema pale uchunguzi huo utakapokamilika,  taarifa zake zitawasilishwa Serikalini kwa hatua za kuupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro huo.

Alisema  kazi za Ulinzi wa nchi ni muhimu katika mustakabali wa usalama wa taifa,  hivyo akawataka wananchi kuelewa kuwa hata maeneo yanayoonekana kuwa wazi , kuna  shughuli muhimu za kiulinzi na  hivyo akabainisha umuhimu wa wananchi kuishi mbali na maeneo ya Jeshi.

Aliwataka wnaanchi hao kuwa na subira, na kuahidi Serikali kufanya maamuzi  pale taarifa zitakapowasilishwa serikalini, huku akiwaomba wananchi hao  kuondokana na mivutano.

Aidha , alisema serikali itafuatilia kubaini changamoto ya wananchi wa Dunga Kiembeni bondeni, wanaodai kutoa kiasi cha shilini Milioni 12 kwa ajili  kuungiwa umeme na baada ya kukamilika mchakato wa kuwekewa miundombinu na kuanza kupata huduma  hiyo, hatimae  Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) limefika na kuondoa miundombinu hiyo.

Akizungumza na wakulima wa Bonde la Mpunga Cheju linaloendesha  mradi mkubwa wa uwekaji wa miundo mbinu ya kilimo cha mpunga kwa njia ya Uwagiliaji, alisema pamoja na mradi kuo kupata ttizo la kuchelewa kuanza, kuna matumaini makubwa ya mradi huo kukamilika mwezi April 2022 na kuleta tija kubwa kwa wakulima.

Aliwataka wakulima wa bonde hilo kuondokana na utegemezi wa kuitegemea Serikali kwa kila kitu, ikiwemo kupatiwa pembejeo, na kubainisha kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya kuwawezesha wakulima hao.

Rais Dk. Mwinyi aliuagiza uongozi wa Wizara ya Kilimo kufanya uchunguzi ili kubaini Viongozi waliohusika kuhodhi maeneo makubwa ya kilimo katika bonde hilo na kutaka kufikishiwa taarifa hizo, hatua iliokuja baada ya wananchi kulalamika kuwepo viongozi waliohodhi maeneo makubwa kwa lengo la kujinufaisha.

Aidha, aliutaka uongozi wa Wizara ya kilimo, …….kukutana na wakulima wa bonde hilo ili kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili, huku akiahidi Serikali kusimamia mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.

Katika hatua nyengine, Rais Mwinyi alikaguwa barabara mbali mbali za ndani zilizomo katika Jimbo la Uzini na Chwaka, ikiwemo barabara ya Kiboje – Miwani – Kizimbani (km 7.2), Mgenihaji – Kwambani(km 2) pamoja na Tunguu – Ndijani kwa Baniani yenye urefu wa kilomita 7.8, ambazo kupitia Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022 zitakuwa miongoni mwa barabara 220 zitakazojengwa kwa kiwango cha Lami.

Akizungumza kwa nyakati tofauti  na wananchi  hao, alisema barabara ni nyenzo muhimu  sana katika kuharakisha kasi ya maendeleo, huku akiwawahakikishai wananchi kutokea mabadiliko makubwa ya kimaendeleo baada ya miradi hiyo kukamilika.

Aliwataka wananchi hususuan wale wenye miti mikubwa ilio karibu na barabara hizo kuikata ili miradi hiyo iweze kukamilika na kuondokana utamaduni  wa kudai fidai, jambalo ambalo baadhi ya nyakati Serikali hushindwa kugharamia na miradi hiyo kushindwa kutekelzwa.

Aidha, aliwataka wananchi kuondokana na utaratibu wa kujenga karibu na eneo lililotengwa kwa ajili ya  upanuzi wa barabara na kubainisha jambo hilo huzorotesha azma ya serikali ya kuwapatia wananchi huduma hiyo.

Akigusia kero mbali mbali za wananchi  zilizojitokeza katika maeneo tofauti aliyotembelea, Dk. Mwinyi aliwapongeza walimu wanaojitolea kwa uzalendo wao na kusema Serikali itachukua itatoa kipaumbele kwao, pale ajira zitakapotolewa na serikali.

Dk. Mwinyi,  alisema Serikali  itaendelea kufanya wajibu wake wa kushughulikia miradi mikubwa ya kijamii, ikiwemo kuimarisha huduma za maji safi na salama, elimu pamoja na upatikanaji wa huduma za afya.

Aliwataka wananchi kuvuta subira wakati Serikali inaaazimia kuja na mpango wa Bima ya Afya ili kuwawezesha wnana chi wote kupata huduma bora za Afya bila ya usumbufu.

Nae, Waziri  wa Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji Rahma Kassim Ali alisema katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022 Serikali imepanga kuzifanyia matengenezo barabara 220 za ndani kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara zilizotemebelewa na Rais Dk. Mwinyi na kuondokana na utaratibu wa ujenzi wa kifusi usio tija.

Aidha, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Malisili na Mifugo Soud Nahoda alisema kukamilika uwekaji wa miundo mbinu ya kilimo cha Mpunga kwa njia ya umwagiliaji katika Bonde la Cheju, kutaongeza kiwango cha uzalishaji mpunga hapa nchini kutoka asilimia 30 na hadi kufikia asilimia 60.


Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.