KAMISHNA
WA USALAMA DHIDI YA MOTO JESUALD IKONKO AKIZUNGUMZA NA BAADHI YA
WAFANYABIASHARA KATIKA ENEO MAARUFU JIJINI DODOMA NYERERE SQUARE JUU YA UMUHIMU
WA KUTUNZA VISIMA VYA MAJI YA KUZIMA MOTO MAPEMA.
Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ZM 2869 CPL Kabuche Tengwa akitoa uchafu katika moja ya visima vya vya kuzimia moto vilivyofukiwa katika ukaguzi uliofanyika leo Jijini Dodoma.
Dodoma 16 Julai, 2021.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limefanya ukaguzi wa visima vya maji ya
kuzima moto (Fire Hydrants) katika
Jiji la Dodoma leo 16 Julai, 2021. Waliombatana katika ukaguzi huo ni Kamishna
wa Utawala na Fedha Mbaraka Semwanza, Kamishna wa Usalama dhidi ya Moto Jesuald
Ikonko, Mwenyeji wa Msafara huo ambaye ni Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji (M)
Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACF Julishael Mfinanga pamoja na Maafisa
na Askari kutoka Makao Makuu ya Zimamoto na Ofisi ya Kamanda wa Mkoa.
Ukaguzi huu umefanyika ili kujiridhisha na hali ya visima hivyo ambavyo
husaidia wakati wa shughuli za uzimaji moto. Katika ukaguzi huo Viongozi hao
waligundua mapungufu mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya visima hivyo
kufukiwa na uchafu kutokana na shughuli mbalimbali zinazoendelea katika maeneo
husika na watu kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wake, vingine kutokuwa na maji kabisa kutokana na miundombinu
chakavu.
Viongozi hao walitumia nafasi hiyo kuzungumza na wananchi wanaofanya
shughuli zao jirani na visima hivyo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha umuhimu wa
kutunza visima hivyo. Akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara katika eneo
maarufu lijulikanalo kama Nyerere Square, Kamishna Ikonko aliwataka
wafanyabiashara kuvitunza visima hivyo ili kuweza kusaidia pale ambapo uhitaji
wa maji utatokea wakati wa zoezi la kuzima moto katika maeneo mbalimbali
katikati ya Jiji la Dodoma.
“Niwaombe wafanyabiashara katika
eneo hili kuendelea kuvitunza visima hivi maana ndio sehemu tunayoweza
kukimbilia kuchukua maji linapotokea janga la moto katikati ya Jiji letu la
Dodoma” alisema Kamishna Ikonko.
Naye Kamishna Semwanza aliagiza ofisi ya Kamanda wa Mkoa kuhakikisha
wanafanya ukaguzi wa visima hivyo kila wakati ili kuondokana na changamoto ya
Maji wakati wa matukio ya moto.
Ukaguzi huo ulifanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Nyerere Square,
Hospitali Kuu ya Jiji la Dodoma “Dodoma General Hospital”, Chuo cha Mtakatifu
John pamoja na Area D.
(Picha zote na Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji)
No comments:
Post a Comment