Habari za Punde

Gawio la Asilimia Mbili ya Mapato ya Manispaa ya Magharibi “A” Unguja ni Kichecheo Kikubwa cha Kuwaletea Maendeleo Watu Wenye Mahitaji Maalum Katika Wilaya Hiyo.

Na Ali Issa -Maelezo 11/8/2021

Afisa Tawala  Wilaya ya Magharibi “A”, Dk. Saidi Mrisho amesema gawio la asilimia mbili ya mapato ya Manispaa ya Magharibi “A” ni kichecheo kikubwa cha kuwaletea maendeleo watu wenye mahitaji maalum katika wilaya hiyo.

Amesema hali hiyo ni yakufurahisha na kupongezwa kwani itaondoa changamoto zinazowakabili walemavu ambao wanahitaji kupewa kipaumbele.

Ameyasema hayo huko Mwera Wilayani, wakati akizindua kamati ya Watu wenye Ulemavu Magharibi “A”, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A” Suzan Peter Kunambi ambae ni mwenyekiti wa kamati hiyo.

 Alisema kuwa, fursa hiyo ni haki yao ya msingi pia agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Hussen Ali Mwinyi katika jitihada za kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu nchini.

Alieleza kuwa, mpango huo ni mwema hivyo  kamati lazima iwe makini katika kuitumia fursa hiyo ili kuondoa changamoto zinazowakabili watu hao.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Magharibi “A” Amour Ali Abdalla, amesema matumizi ya pesa hizo zitamika ipasavyao kwa  kufuata taratibu na kanuni za kifedha  zilipangwa na serikali.

Amesema watu wenye mahitaji maalumu katika wilaya hiyo na sehemu nyengine wanafursa sawa kikatiba na kisheria katika kupata haki zao, hivyo gawio lililopangwa litawafika walengwa kama ilivyokusudiwa.

“Fungu la asilimia mbili lipo na limeshapita mwaka hivyo wakati wowote zinapatikana muhimu ni kufuata taratibu za kifedha na matumizi kama Serikali ilivyoagiza”, alisema Kaimu Mkurugenzi.

Mapema Katibu wa Kamati ya Watu wenye Ulemavu Yumna Ali Mwinjuma, alisema kuwa kamati hiyo imezingatia mahitaji ya watu hao kwani watapata fursa nyingi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha aliwataka wanakamati kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao ili kutimiza azma iliyowekwa ya kuwaletea maendeleo watu wenye Ulemavu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.