Habari za Punde

Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu kwa wote kutoka Qatar kusaidia kuwarejesha watoto watoro maskulini

 Na Maulid Yussuf WEMA.

ZANZIBAR

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetiliana saini na Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu kwa wote (Education for All) kutoka Qatar mkataba wa makubaliano ya Mradi wa kuwarejesha watoto waliotoroka Skuli  ili waweze kupata haki yao ya Elimu.

Mkataba huo umesainiwa na katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar bwana Ali Khamis Juma na Mwakilishi wa EAC kutoka Qatar Dkt. Mary Pigoz.

Akizungumza baada ya utiaji wa saini mkataba huo, katika ukumbi wa Hoteli ya Park Hayyat Mjini Unguja, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema Wizara itahakikisha inasimamia suala la Elimu ili kuhakikisha watoto wanapata haki yao hiyo.

Amesema  watoto wote wanahaki ya kupata elimu ya lazima kuanzia ngazi ya maandalizi hadi kidatu cha nne, hivyo mradi huo pia utasaidia kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.

Amesema Wizara imejitolea kwa kushirikiana na  Serikali za Mikoa, jamii na wazazi na wadau wa elimu ili kuhakikisha watoto wote waliotoroka  wanarudi Skuli ili kuendelea kupata elimu yao ya lazima.


Amesema watoto hao wamekua wakitoroka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo  hali ngumu ya maisha na maradhi hali ambayo inaweza kutatuliwa.

Nae katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Ali Khamis Juma amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha wanawasaidia watoto waliotoroka Skuli wenye umri wa kuwa Skuli, wanawarudisha na kuhakikisha wanasoma katika mazingira mazuri na salama.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu kwa Mtoto, Elimu kwa wote (EAC ) kutoka nchini  Qatar Dkt. Mary Pigozzi amesema  lengo lao ni kuhakikisha hakuna mtoto anaekosa elimu ya lazima, hivyo watashirikiana na Wizara ya Elimu Zanzibar ili kuona malengo yao yanafikiwa.


Amesema Zanzibar ni nchi moja wapo kati ya nchi nne zinazotarajia kupata Mradi wa kuwarejesha Skuli watoto ambao bado wana  umri wa  kupata elimu, ikiwa tayari nchi mbalimbali duniani wamefanikiwa katika kuwarejesha watoto skuli.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania bibi Shalin Bahu Guna amesema  kwa mashirikiano ya pamoja watahakikisha watoto wanarudi skuli hasa mtoto wa kike kwani wao wanaonekana kutokuwa na msukumo mkubwa hasa kwa familia.


Mkurugenzi Idara ya Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Khalid Masoud Waziri amesema  Wizara imejipanga kuimarisha miundombinu katika elimu ili kuhakikisha watoto  wanasoma katika mazingira mazuri.

Jumla ya dola milioni tatu zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya mradi wa kuwarejesha watoto Skuli ambapo kiasi ya watoto Elfu 36 wanatarajiwa kurejeshwa Skuli chini ya ufadhili wa Shirika la UNICEF pamoja na Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu kwa wote (Education for All) kutoka Qatar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.