Habari za Punde

WATAKAOLALA GESTI SIKU YA SENSA WATAFUATWA KUHESABIWA

Na.Richard Mwaikenda. Dodoma.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa akifafanua jambo wakati wa mkutano na wadau wa Mkoa wa Dodoma wa kuhamasisha na kutoa elimu juu ya sensa ya watu na makazi uliofanyika Agosti 18  jijini Dodoma.

Kamishna wa Sensa, Spika mstaafu, Anne Makinda akielezea umuhimu wa sensa hiyo na kuwasihi watanzania siku hiyo ya sensa wajitokeze kwa wingi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akijadiliana jambo na mmoja wa wageni waalikwa.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma, Mwanahamisi Munkunda akielezea jinsi walivyonufaika na sensa ya majaribio iliyofanyika wilayani humo.

Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo.Mbunge wa Mpwapwa George Malima akichangia mada wakati wa mkutano huo.

Mbunge wa Viti Maalumu ambaye pia ni msanii, Khadija Taya 'Keisha' akichangia mada wakati wa mkutano huo ambapo pia aliomna kuwashirikisha watu wenye ulemavu kwenye kamati za sensa,

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwanfupe akielezea umuhimu wa kutoa elimu ya sensa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waieneze kwa wazazi.

Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzi akielezea kuikubali sensa hiyo na kuahidi kuwahamasisha wamachinga siku ya sensa kujitokeza kwa wingi.

Mwenyekiti wa Bodaboda/Bajaji Mkoa wa Dodoma,  na Makamu Mwenyekiti Taifa, Keneth Chimoti akichangia mada na kuunga mkono sensa na kuahidi kuhamasisha waendesha Bodaboda/Bajaji ili wajitokeze kwa wingi kuhesabiwa siku hiyo ya Sensa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatma Mganga (Kulia) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Bahi ambaye pia ni kiongozi wa wakuu wa wilaya wa mkoa huo, Mwanahamisi Munkunda wakati wa mkutano huo. 

WATU wote watakaolala nyumba za wageni (Gesti) Siku ya sensa ya Watu na Makazi watafuatwa huko huko na makarani  kuhesabiwa.

Hayo yamesemwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa wakati wa mkutano na wadau wa Mkoa wa Dodoma wa kuhamasisha na kutoa elimu juu ya sensa ya watu na makazi.

"Watu wote watakaokuwa wamelala siku hiyo Guest, hotelini  makarani watakwenda kuwahesabu ikwemo na wale wote watakao safiri maeneo mbalimbali," amesema Dkt Chuwa.

Amesema kuwa siku hiyo  usiku majira ya saa 6 na dakika moja makarani wa sensa wataanza kuhesabu kwenye Gesti, mahotelini, stendi na maeneo mengine yanayohusisha safari.

Aidha, Dkt. Chuwa amesema kuwa wageni wote kutoka mataifa mbalimbali ambao siku hiyo ya sensa watakuwa wamelala nchini watahesabiwa na kuchambuliwa baada ya sensa kujua idadi yao na idadi kamili ya wazawa.

Amesema kuwa,licha ya sensa hiyo kuhesabu watu wakiwemo wenye aina mbalimbali za ulemavu, watoto wa mitaani, lakini pia itagusa sekta nyingi kama vile makazi ya watu zikiwemo nyumba na aina mbalimbali za mifugo.

Mkutano huo wa wadau ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ya Mkoa huo, Anthony Mtaka ulihudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Wengine ni Kamishna wa Sensa, Spika mstaafu, Anne Makinda, wabunge wa mkoa huo, wakuu wa wilaya, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa mabaraza ya wazee na taasisi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu.

Sensa WATAKAOLALA GESTI  SIKU YA SENSA WATAFUATWA KUHESABIWA itafanyika Agosti 2022 na kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania,  Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.