Habari za Punde

Viongozi Wetu wa Kisiasa Zanzibar Waliokaa Meza Moja na Kuleta Maridhiano ni Kitu Kizuri na Kinachofaa Kupongezwa.

Na.Mwanajuma Juma.

KILA panapokuwepo tafauti ya aina moja au nyengine, iwe katika familia, jamii au nchi maridhiano yamebaainisha kuwa ndio njia bora ya kuwafikisha watu katika hali ya kuelewana na kujipatia maendeleo, raha na furaha.

Yanapokosekana maridhiano huwa vurugu na gharama za sutofahamu huwa kubwa na wakati mwengine watu kupoteza mali na hata maisha.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ametuhimizaa kushirikiana katika kila jambo la kheri ni vizuri siku zote kila mtu kufanya juhudi ya kuwepo maridhiano kila pahala na kuendeleza mazuri waliotuachia wahenga na viongozi wa sekta mbali mbali.

Hatua ya viongozi wetu wa kisiasa wa Zanzibar waliokuwa wanatafautiana sana kuamua kukaa meza moja na kuleta maridhiano ni kitu kizuri na kinachofaa kupongezwa.

Kwanza ni kutekeleza maamrisho ya mola na jengine ni kukubali kujifunza athari na hatari ya kutoelewana tulizoshuhudia sio hapa kwetu, bali pamoja na kwa majirani zetu na nchi nyengine.

Kutokuwepo maridhiano na kushabikia vuta nikuvute ndiko kulikopelekea kuwepo mapigano katika nchi mbali mbali na hata kuzusha vita, vikiwemo Vita vya Kwanza vya Dunia (1914-1918) na Vita vya Pili vya Dunia (1938-45).

Wazanzibari wengi nao walijikuta wametumbukizwa katika vita hivi na kushiriki nje ya visiwa hivi kutokana na Zanzibar wakati ule kuwa himaya ya Uingereza.

Tokea kupatikana maridhiano ya kisiasa Zanzibar, viongozi wetu wamekuwa wakihimiza mara kwa mara umuhimu wa kuyaenzi maridhiano yaliyokuwepo.

Hili limefanyika katika majukwaa na hafla mbali mbali na hata misikitini. Kwa kweli ni wajibu wa kila Mzanzibari, bila ya kujali mtazamo wake wa kisiasa au kuhesabu yaliyopita kufanya kila juhudi kuhakikisha maridhiano yaliyopatikana yanadumu na kuimarika.

Hii ndio njia pekee, sahihhi na salama ya kuendeleza amani na utulivu katika nchi yetu na hatimaye kujipatia maendeleo yenye raha na furaha.

Kwa hivyo, kila mtu anapaswa kufuata nyayo za viongozi wetu ambao kwa makusudi walikutana na kutafuta maridhiano kwa maslahi ya Zanzibar na watu wake.

Viongozi wetu waliamua kupata maridhiano baada ya kuona siasa za chuki, hasama, kugombana na hata kupigana hazina faida kwa nchi na wananchi kwa ujumla.

Hivi karibuni, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.Mhe.Othman Masoud Othman, alikutana na ujumbe wa Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), na miongoni mwa masuala aliyoyapa umuhimu katika mazungmzo hayo ni kuhimiza kuimarishwa kwa maridhiyano yaliyofikiwa.

Masoud alisema suala hilo la kuhamasishana kuhusu maridhiyano liwe sio tu kwa kundi maalumu la watu, bali kwa watu wote na kusistiza kwamba kufanya hivyo kutasaidia  kujenga amani ya kweli kwa vizazi vya sasa na baadae.

Alisema maridhiano ni mtaji na raslimali muhimu inayopelekea kupatikana  Amani na endapo yakitoweka nchi haiwezi kuimarika.

Hatimaye nchi hutumbukia katika machafuko yanayokuwa na gharama kubwa za maisha, ikiwa pamoja na kuongezeka  watu wenye ulemavu. “Ninapenda niwape changamoto kidogo kama ilivyo kwa jumuiya nyingine. Mkahamasishe maridhiano yatakayopelekea ujenzi wa amani ya kweli kama ajenda muhimu, kwani yakija machafuko siyo tu yatawaathiri watu wenye ulemavu, bali yataongeza hata huo ulemavu wenyewe”, alisisitiza
Othman.

Othman alibainisha kuwa mambo mengine yanayochangia ongezeko la watu wenye ulemavu ni pamoja na ongezeko la maradhi yasiyoambukiza, dawa za kulevya na kutojali sheria za usalama barabarani.“Tukiwa sote tunajenga nyumba moja hatuna haja ya kuona tunasambaratika kwa sababu tu hakuna maelewano ambayo uwepo wake kunasaidia kuiletea maendeleo mazuri nchi”, alisitiza.

Kwahivyo, aliwataka watu wenye ulemavu kujiona sawa na watu wengine katika kuhakikisha wanasimama imara katika kuhamasisha maridhiyano katika nchi.

Viongozi wa SHIJUWAZA, Makamu Mwenyekiti na Mratibu, Ali Omar Makame na Bakar Omar Othman, walielezaa kwamba uwepo wa Shirikisho hilo ni juhudi za pamoja za kupigania haki, fursa na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu ili kuimarisha ustawi bora wa jamii Unguja na Pemba.

Viongozi hao waliishukuru Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa kuunga mkono juhudi za kuwakomboa watu wenye ulemavu, licha ya changamoto nyingi zinazowakabili, zikiwemo za udhalilishaji na ugumu wa maisha.

Kikao hicho kiliwajumuisha viongozi mbali mbali, akiwemo Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.Dkt Omar Dadi Shajak, aliyeelezea juhudi zinazochukuliwa na wizara husika za pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano katika kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.

Maridhiano yametoa mwanga wa matumaini mema, hasa baada ya joto la chuki za kisiasa na uhasama sio kupowa tu, bali kuonekana linalotokea. Lililo muhimu sasa ni kila mmoja kutoa mchango ili safari yetu iwe ya kusonga mbele na sio kurudi nyuma na hili liendelezwe kwa kuheshimu katiba, sheria na kwa heshima na adabu.

Historia haitawasahau waliochangia kufikiwa maridhiano hayo ambayo hatimaye watu wa Zanzibar wameanza, kama walivyokuwa wazee wao hapo zamani, kubakia kitu kimoja na kushurikiana wakati wa dhiki na furaha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.