Habari za Punde

Utawala Bora Ni Ufunguo Wa Maendeleo Zanzibar - Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mhe Masoud.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza na ngeni wake Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Marekani Bw.Paul Grove, aliofika ofsini kwa Makamu kwa mazungumzo na ushirikiano na uhusiano katika sekta mbalimbali.  
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza na ngeni wake Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Marekani Bw.Paul Grove, aliofika ofsini kwa Makamu kwa mazungumzo na ushirikiano na uhusiano katika sekta mbalimbali.  
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Marekani ukiongozwa na Bw.Paul Grove, walipofika ofsini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa mazungumzo na ushirikiano na uhusiano katika sekta mbalimbali.  

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema nchi hii inayo fursa kubwa ya maendeleo pindipo itazingatia misingi ya utawala bora, matumizi sahihi ya rasilimali, kuidumisha serikali ya umoja wa kitaifa na mahusiano mema ya kimataifa.


Mhe. Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani, Mjini Zanzibar, mbele ya Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Bunge la ‘Senate’ la Marekani, iliyofika kumtembelea na kujadili mambo mbali mbali ya maendeleo ikiwemo hali ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (GNU).

Mhe. Othman ameeleza kuwa ni faraja kubwa kufikiwa na ujumbe huo ikizingatiwa kwamba Marekani na Zanzibar wamekuwa na mahusiano ya kidiplomasia kwa miaka mingi tangu kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Aidha, ameubainishia ujumbe huo hatua za makusudi za kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ambazo ni pamoja na mapendekezo ya mageuzi ya kujenga ufanisi na uwepo wake bila ya kutegemea ni kiongozi gani aliyepo madarakani.

Akisisitiza haja ya umoja na mashirikiano katika kufikia maendeleo ya nchi yoyote Mhe. Othman alisema, “kwa kiasi kikubwa wenzetu wamekuwa na uzoefu katika kufanikisha changuzi za kistaarabu, utaalamu na uweledi, na kwa nchi kama Zanzibar, hizo ni kati ya fursa muhimu za kujifunza kutokea Taifa hilo lililoendelea”.

Kikao hicho kimejaribu kukumbusha mengi ya kujivunia, kati ya pande mbili hizo kama sehemu ya mahusiano mema, ukiwemo Mipango ya Marekani ya kukabiliana na Changamoto (MCC) ambao kwa hapa Zanzibar pamoja na miradi mingine ikiwemo ya sekta za elimu na afya, ulisaidia pia miundombinu ya umeme wa chini ya bahari kutokea Tanzania Bara.

Ujumbe huo umepongeza juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Zanzibar katika kukuza na kuendeleza mahusiano mema ya kidiplomasia na Marekani.

Kiongozi wa Ujumbe huo, Bw. Paul Grove ametoa ushauri kwa Zanzibar akisema kuwa, ili kufanikisha maendeleo ya kweli ni vyema kuushirikisha umma kwa upana wake, na hilo litawezekana pindipo mamlaka zitashirikiana kikamilifu na asasi za kijamii.

Kiongozi huyo amebainisha kuwa Marekani inaelewa namna janga la Uviko-19 lilivyoathiri uchumi, hasa wa Nchi kama Zanzibar inayotegemea utalii, hivyo haitosita kusaidia katika hali tofauti ikiwemo utoaji wa chanjo.

Sambamba na hayo amesema Marekani itahamasika kuendelea kuisaidia Zanzibar pindipo itabaini kuwepo kwa nia ya dhati katika utekelezaji wa mipango makini ya maendeleo, utekelezaji wa misingi ya utawala na pia mageuzi ya kweli ya kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.