Habari za Punde

ZEC yaaswa 'Shirikianeni na Taasisi za kiraia'

Bi Hawra Mohammed Shamte akiwasilisha ripoti ya utafiti  juu ya utekelezaji wa sera ya jinsia ya Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC katika ofisi za Tume hio Maisara mjini Unguja.


Mkuu wa Kurugenzi ya Rasilimali Watu Tume ya uchaguzi, Mipango na Uendeshaji Tume ya uchaguzi Zanzibar Saadun Ahmed Khamis akifafanua jambo mara baada ya kuwasilishwa ripoti hio.


Wajumbe mbali mbali kutoka Asasi za kiraia na Tume ya ucaguzi wakifuatilia uwasiliswaji wa ripoti hio katika ofisi za Tume zilizopo Maisara mjini Unguja.


Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ


Kwa lengo la kuongeza idadi kubwa ya ushiriki wa wanawake katika nafasi mbali mbali za uongozi visiwani Zanzibar,tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeshauriwa kushirikiana na Asasi za kiraia ili kuongeza ushawishi kwa vyama vya siasa kuwashajihisha wanawake kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.


Ushauri huo ulitolewa na Mjumbe kutoka Jukwaa la Mtandao wa Asasi za Kiraia visiwani Zanzibar  Bi Hawra Mohammed Shamte wakati akiwasilisha mada ya utekelezaji wa Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi maalum katika kikao kilichofanyika Afisi za Tume hio Maisara Mjini Zanzibar.


Alisema, Tume ya Uchaguzi ilianzisha Sera ya jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi maalumu mwaka 2015 kwa lengo la kuhakikisha makundi yote wakiwemo Wanawake na Watu wenye ulemavu wanashiriki katika hatua zote za Uchaguzi ikiwemo kugombea katika chaguzi zinazoendeshwa Zanzibar.


Alendelea kusema kuwa, Jukwaa la Mtandao wa Asasi za Kiraia (CSOs Network Forum) ambalo liemundwa na TAMWA, Jumuiya ya Waandishi wa Habari wenye ulemavu na Mtandao wa Asasi za Kiraia wameipitia Sera na kufanya utafiti wa utekelezaji wake kwa kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu na kuona changamoto mbali mbali ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi.


Akitaja miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na vyama vya siasa kutotoa kipao mbele kwa wanawake kugombe majimbo ambayo wanahisi wana nguvu ya kushinda badala yake majimbo hayo huwekwa wagombea wanaume zaidi.


Akichangia mada katika mkutano huo Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa alisema  licha ya uwepo wa Sera mbali mbali katika tume hio lakini kumekua na changamoto ya utekelezaji wa sera hizo zaidi inapokaribia kipindi cha uchaguzi.


Alisema ili sera hizo ziweze kufanya kazi ipasavyo hakuna budi kuwe na utaratibu maalumu wa kufanya utafiti kuona umefikia wapi na unahitaji kitu gani kufikia malengo zaidi.


Sambamba na hayo alisema ili hayo yote yaweze kufanikiwa hakuna budi kuendeleza  mashirikiano baina ya Tume hio na Asasi za kiraia.


Kwa upande wake mkuu wa kurugenzi ya elimu kwa wapiga kura Juma Sanifu alisema licha ya uwepo wa sera ya Tume hio kuliku na kasoro mbali mbali katika jamii wengi wao walishindwa kufaamu namna sera hio inavofanya kazi.


Akitolea mfano alisema katika ucaguzi uliopita alimuona Askari polisi akimtoa kwenye foleni mtu mwenye ulemavu kwa madai ya kuchelewa wakati alipaswa kupewa kipao mbele zaidi ili aweze kutekeleza haki yake hio ya kikatiba.


Kwa upande wake Mkuu wa Kurugenzi ya Rasilimali Watu, Mipango na Uendeshaji Saadun Ahmed Khamis aliwaomba Wadau  wa Uchaguzi wakiwemo vyama vya Siasa na Asasi za Kiraia kuipitia Sera hiyo na kuwasilisha changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa utekelezaji wake.


Sambamba na hayo aliwapongeza Chama cha Waandishi wa habari wanawake kwa kuwa Taasisi ya mwanzo kuipitia na kuifanyia kazi Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi ya Kijamii yam waka 2015 iliyoanzishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.