Habari za Punde

Benki ya NMB Yaaza Kutoa Mikopo ya Riba Nafuu Kwa Wateja Wake Katika Sekta ya Kilimo,Ufugaji na Uvuvi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa mikopo ya riba nafuu kwa wateja katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo zaidi ya Sh. Bilioni 100 zimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara, Isaac Masusu na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi. 
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mikopo ya riba nafuu kwa wateja katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo zaidi ya Sh. Bilioni 100 zimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo. Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna. (Na Mpiga Picha Wetu).

Benki ya NMB inapenda kuwatangazia wateja wake wote walioko kwenye mnyororo mzima wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi kuwa, kuanzia tarehe 15.10.2021 itaanza kutoa mikopo ya riba nafuu. Mikopo hiyo itatolewa kwa kiwango cha riba isiyozidi asilimia 10% kwa mwaka. 

Wanufaika wa mikopo hii ya riba nafuu ni wakulima, wauzaji wa pembejeo, watoa huduma, wajasiriamali na wasindikaji wadogo na wa kati wanaojishughulisha na shughuli zote katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Zaidi ya Shilingi Bilioni 100 zimetengwa kwaajili ya kutoa mikopo nafuu kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Benki ya NMB inachukua hatua hii ili kupanua wigo wa wadau wengi katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kupata mikopo yenye riba nafuu ambayo itaongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.

Mteja sasa ataweza kuwa na unafuu wa gharama ya mkopo na hivyo kuweza kujitengenezea faida zaidi. Faida hiyo inaweza kutumika kuongeza uzalishaji wa chakula, malighafi za viwanda na kuchagiza maendeleo ya viwanda nchini.

Ni matarajio ya benki ya NMB kuwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati katika tasnia hii wataitumia fursa hii adhimu kujipatia mikopo yenye gharama nafuu na kujiongezea kipato ili kujenga uchumi wa nchi.

Benki itazingatia masharti ya utoaji wa mikopo hii nafuu kwa kuzingatia taratibu za ukopeshaji ikiwemo kiwango cha juu cha mkopo cha TZS 1 Bilioni kwa mkopaji mmoja. Mkopaji huyu anaweza kuwa mtu binafsi, chama cha ushirika, kampuni au taasisi yeyote itakayokidhi masharti ya ukopeshaji. Benki inatoa wito kwa walengwa kuwasiliana na mtandao wake wa zaidi ya matawi 225 yaliyo enea nchi nzima ili kuweza kupata huduma za mikopo hii ya riba nafuu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.