RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Mhe. Muumin Khamis Kombo kuwa Jaji wa
Mahkama Kuu Zanzibar, hafla hiyo ya uapisho imefanyika katika ukumbi wa Ikulu
Jijini Zanzibar leo 30-10-2021, na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi leo
amewaapisha watendaji mbali mbali
aliowateuwa Oktoba 29, mwaka huu kushika nyadhifa zao katika sekta ya Sheria.
Katika hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amemuapisha Muumin Khamis Kombo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar pamoja na Salma Ali Hassan kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP).
Aidha, amemuapisha Mwanamkaa Abdulrahman Mohammed kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Katika hafla hiyo Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walihudhuria, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Talib Mwinyi Haji, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab pamoja na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Watendaji wa Mahakama, Viongozi wa Kisiasa pamoja na wana familia.
Wakizungumza baada ya ya hafla hiyo, watendaji hao wameahidi kushirikiana na watendaji wengine wa Mahakama katika kuharakisha usikilizaji wa kesi ili wananchi waweze kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, wamesema watashirikiana na jamii, Asasi zisizo za Kiserikali na zile za Kiserikali ili kuhakikisha kunakuwepo mikakati na mifumo bora katika mapambano dhidi ya vitendo vya Udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Kitengo cha habari,
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment