Habari za Punde

KMKM Yatwaa Ubingwa Mchezo wa Riadha Zanzibar.

Na Mwajuma Juma. Unguja. 

TIMU ya Riadha ya  Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM imetwaa ubingwa wa Zanzibar katika michuano ya  klabu bingwa Zanzibar yaliyomalizika jana visiwani Zanzibar.

KMKM  ilifanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya kuwatupa ndugu zao wa JKU ambao walishika nafasi ya pili na kaka zao Nyuki  walishika nafasi ya tatu.

Bingwa huyo ambae akiondoka na kombe la kitita cha shilingi 700,000 alipata  medali 31 zikiwemo za dhahabu 12, fedha 10 na shaba tisa.

Akitangaza matokeo ya washindi hao Katibu wa Kamati ya Ufundi ya Chama cha  Riadha Zanzibar ZAA Faida Salmini Juma, alisema JKU ambao ni washindi wa pili   walipata medali tisa za dhahabu, 12 fedha na shaba tisa.

Kwa upande wa timu ya Nyuki walioshika nafasi ya tatu ambao walipata medali sita za dhahabu, fedha mbili na shaba tano.

Mgeni rasmi katika michuano hiyo alikuwa ni Katibu wa Shirikisho la Soka Zanzibar ZFF Hussein Ahmada ambae alikabidhi zawadi kwa washindi hao.

 Mshindi wa pili alipata kikombe na shilingi 500,000 na wa tatu akaondoka na kikombe kidogo na shilingi 300,000.

Katika mashindano hayo timu ya Mafunzo ilitangazwa kuwa timu yenye nidhamu na kukabidhiwa shilingi 100,000.

Jumla ya timu tisa zilishiriki michuano hiyo ambayo yalianza kutimua vumbi lake Novemba 27 mwaka huu.

Klabu nyengine ambazo zimeshiriki michuano hiyo ni Polisi, Kidoti, Chemchem, Lumumba, Kidoti, MUKIJOPE na Uhamiaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.