Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Mwakilishi wa UNICEF Ofisi ya Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Mwakilishi  wa UNICEF anayefanyika Kazi zake Ofisi ya Zanzibar.Bi. Laxmi Bhawani.mazungumzo hayo yamefanyika  katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa  Jarida la UNICEF  likiwa na ujumbe wa ‘Maliza Ukatili na Udhalilishaji Dhidi ya Wanawake na Watoto Zanzibar’ na Mwakilishi wa UNICEF wa Ofisi ya Zanzibar Bi. Laxmi Bhawani, wakati wa mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwakilishi wa UNICEF anayefanyia kazi zake Ofisi ya Zanzibar Bi.Laxmi Bhawani, baada ya kumkabidhi Jarida la UNICEF linalozungumzia  Maliza Ukatili na Udhalilishaji Dhidi ya Wanawake na Watoto Zanzibar, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Kiongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ofisi za Zanzibar, Laxm Bhawani  kwa kazi kubwa na nzuri  inayofanywa na Ofisi hiyo na akamhakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kumuunga mkono ili kufikia mafanikio katika maeneo anayofanyia kazi.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Jijini hapa, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Ofisi za Zanzibar Laxmi Bhawani.

Alisema Ofisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuhakikisha huduma mbali mbali ikiwemo za Afya na Elimu zinaimarika hapa nchini, sambamba na kuondokana na umasikini pamoja na utapia mlo kwa  watoto.

Alisema upatikaji wa lishe kwa watoto ni jambo muhimu na akabainisha kazi kubwa inayopaswa kufanyika kufanikisha jambo hilo, kwa kuzingatia takwimu zilizopo za watoto wenye utapia mlo.

Alisema katika kuimarisha huduma za Afya, Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika uwekaji wa miundo mbinu katika sekta hiyo pamoja na kuwajengea uwezo watendaji wake.

Dk. Mwinyi, alitolea mfano wa dhamira  ya Serikali ya kujenga Hospitali katika Wilaya zote Unguja na Pemba na hivyo kuwepo mahitaji makubwa ya wafanyakazi wa huduma za Afya  katika nyanja mbali mbali.

 

Rais Dk. Mwinyi, alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, imekuwa ikifanya juhudi kuona kwa namna gani itaweza kuimarisha kiwango cha elimu hapa nchini kupitia sera ya elimu iliopo.

                                                                

Mapema, Kiongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, Ofisi ya Zanzibar Laxmi Bhawani, alimueleza Rais Dk. Mwinyi  masuala mbali mbali yanayotekelezwa na Ofisi yake, ikiwemo ya kufanikisha Programu ya Ulimwengu ya kuwarejesha watoto shule, mitaala ya walimu ya kuinua viwango vya ufundishaji, sambamba na   hatua ya kushirikiana na  taasisi mbali mbali, ikiwemo  Mradi w akunusuru Kaya maskini (TASAF)  katika kufanikisha mpango wa kupunguza umasikini nchini.

 

 

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.