Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Wawekezaji Jijini Durban Afrika Kusini.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Benki ya Afrexim ukiongozwa na Kiongozi Mkuu wa Benki hiyo Bw.Amr Kamel na (kulia kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.Mhe.Omar Said Shaban,mazungumzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa jengo la mikutano la ICC Jijini Durban,baada ya kumalizika kwa mkutano wa ufunguzi wa mkutano wa Maonesho ya Wafanyabiashara wa Nchi za Afrika,uliofanyika katika ukumbi wa ICC Jijini Darban Afrika Kusini
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Wawekezaji kutoka Nchini Misri ukiongozwa na Kiongozi Mkuu ya Kampuni ya Elsewedy.Mhandisi Ahmed  El Sewedy na (kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.Mhe Omar Said Shaban,mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya “The Oyster Box” Jijini Durban Afrika Kusini, baada ya kumalizika kwa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Maonesho ya Wafanyabiashara wa Nchi za Afrika

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya El sewedy ya nchini Misri na kuukaribisha kuja kuekeza Zanzibar kutokana na fursa mbali mbali ziliopo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Elsewedy yenye Makao makuu yake nchini Misri ambapo uongozi huo uliongozwa na Kiongozi Mkuu wa Kampuni hiyo Injinia Ahmed  El Sewedy, mazungumzo yaliyofanyika katika hoteli ya “ The Oyster Box” Jijini Durban.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi wa Kampuni hiyo kwamba Zanzibar ina dhamira ya kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi ambayo yatajumuisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya bandari, barabara, uimarishaji wa sekta ya nishati, ujenzi wa hoteli za kitalii, na sekta nyengine za huduma kama vile afya na elimu.

Alifahamisha kwamba kupitia mpango Serikali wa kuendeleza uchumi wa Buluu kuna fursa nyingi katika mpango huo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli za kisasa za kitalii, ujenzi wa bandari za kisasa zenye kutoa huduma mbali mbali, uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na uvuvi wa bahari kuu.

Vile vile, Rais Dk. Mwinyi alifahamisha kwamba Zanzibar inakaribisha wawekezaji katika visiwa vidogo vidogo ambavyo imevitenga kwa shughuli za uwekezaji.

Aidha, Rais Dk, Mwinyi aliueleza uongozi huo kwamba ili Zanzibar iweze kutekeza dhamira yake ya kuwa kituo muhimu cha biashara muhimu katika ukanda wa Afrika Mashariki, inakaribisha wawekezaji katika sekta za kijamii ambapo inajumisha uwekezaji katika sekta ya elimu na afya.

Alimfahamisha kwamba wawekezaji wengi hivi sasa wamevutiwa kuja kuekeza Zanzibar kutokana na mipango ya Serikali ya kuimarisha mazingira, sheria na sera za  uwekezaji.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliualika uongozi wa Kampuni hiyo kuja kuangalia fursa na kuanza mazungumzo ya awali kwa yale maeneo ambayo watapenda kuekeza.

Nae Kiongozi Mkuu wa Kampuni hiyo, Injinia Ahmed El Sewedy alieleza kuwa wamefurahi kwa kukutana na Rais Dk. Mwinyi na kusema kwamba kwa kipindi kirefu amekuwa akifuatilia na kusikia fursa zilizopo Zanzibar za uekezaji ambapo mazungumzo hayo yamempa mwanga wa ufahamu wa kina kwa yale ambayo amekuwa akiyafuatia na kupata habari kwa namna mbali mbali.

Injinia Sewedy alieleza kwamba Kampuni hiyo tayari imewekeza katika sehemu mbali mbali za Aftika katika sekta mbali mbali za maendeleo kwa hivyo, maeneo yote aliyowaeleza Rais Dk. Mwinyi yanaendana na Sera na Mipango ya Kampuni hiyo.

Alisema kuwa Kampuni yake iko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili iweze kufikia malengo iliyojiwekea huku uongozi huo ukitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kutoa mwaliko huo maalum wa kuitembelea Zanzibar ili kuja kuona fursa zilizpo na kuahidi kwamba kipindi kifupi kijacho ataongoza ujumbe mzito kuja Zanzibar kutembea na kuanza taratibu husika.

Katika mazungumzo hayo viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walishiriki.

Mapema mara baada ya kumaliza ufunguzi wa Mkutano wa Maonyesho ya Biashara baina ya nchi za  Afrika, uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Inkosi Albert Luthuli, KwaZulu-Natal, Jijini Durban, nchini Afrika Kusini Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya Afrexim  inayoshirikiana na nchi kadhaa za Afrika katika kuunga mkono jitihada za nchi hizo katika maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi wa Benki hiyo mipango muhimu ya kiuchumi na kijamii iliyopangwa kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nane anayoiongoza pamoja na fursa za kiuchumi zilizopo kwa wawekezaji.

Nao uongozi huo ulifurahi kupata fursa ya kuzungumza na Rais Dk. Miwnyi na kueleza utayari wa Benki hiyo katika kuunga mkono na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa mikakati  iliyojipangia.

Mara baada ya mazungumzo hayo kwa nyakati tofauti Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini  Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi walieleza mafanikio ya Mkutano huo pamoja na kuipongeza hotuba ya Rais Dk. Mwinyi ambayo ilielezea mipango ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha dhamira ya nchi za Afrika ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina yao inafanikiwa kama ilvyodhamiriwa na  nchi wanachama wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA)  

Rais Dk. Mwinyi ameondoka Jijini Durban, Afrika Kusini leo na kurejea nchini Tanzania baada ya kumaliza  ufunguzi wa Mkutano wa Maonyesho ya Biashara baina ya nchi za  Afrika, ambapo alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.