Habari za Punde

Vyama Vya Mawakili Kutoka Afrika Mashariki Vyapongezwa kwa Jitihada Zao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Jumuiya ya mawakili wa Afrika Mashariki akiwapongeza juu ya jitihada zao wanazozichukua katika kushajihisha utawala wa sheria, Mhe. Hemed katika Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Sea Clif alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi.

Na.Kassim Abdi.OMPR.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amevipongeza vyama vya mawakili kutoka Afrika Mashariki kwa jitihada zao za kufanya kazi pamoja jambo ambalo linasaidia kukuza uwelewa wa masuala ya kisheria katika nchi wanachama.

Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo kwa niaba ya Rais Dk. Mwinyi katika mkutano wa 26 wa vyama vya mawakili vya Afrika Mashariki uliofanyika katika  hotel ya Sea Clif iliopo Kama Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema umoja huo unasaidia kwa kiasi kikubwa kupaza sauti zao sambamba na kubadilishana uzoefu kupitia mafunzo mbali mbali yanayotolewa katika mikutano hio.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais alieleza kuwa kupitia mikutano hio ya vyama vya mawakili mbali na kusaidia kupaza sauti zao lakini pia inasaidia kushajihisha utawala wa sheria na kuruhusu kubadilishana uzowefu kupitia Nchi zilizomo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kupitia Mkutano huo Mhe. Hemed aliuhakikishia umoja wa vyama vya mawakili kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaunga mkono na kuthamini jitihada zinazochukuliwa na wanachama wa umoja huo pamoja na kutambuliwa na uongozi wa ngazi mbali mbali za serikali zilizomo ndani ya Nchi za Afrika Mashariki.

Alifafanua kwamba, kwa vile jukumu la kushajihisha utawala wa sheria haliishii mikononi mwa wanasheria pekee serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua jitihada za maksudi katika kushajihisha suala ilo kupitia katiba ya Zanzibar Kifungu namba 5 cha Katiba ya Zanzibar.

"Zanzibar itakuwa nchi yenye kufuata mfumo wa vyama vingi ambao utazingatia mfumo wa utawala wa sheria, haki za binadamu,Amani,haki na usawa" Alieleza Mhe. Hemed

Alisema kuwa, Pia Katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Kifungu namba Sita inatoa haki za msingi kwa nchi wanachama ikiwemo utawala bora, demokrasia, utwala wa sheria, uwajibikaji pamoja na uwazi.

Kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Nchi Afisi ya Rai, Katiba, sheria Utumishi na Utawala bora Mhe. Haruna Ali Suleiman alisema serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa chama cha Mawakili Zanzibar  katika kuzitatua changamoto zilizokuwepo.

Nae, Rais wa Vyama vya Mawakili Afrika Mashariki Bernard Oundo aliipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua waliofikia katika kustawisha utala bora kwa kuanzisha wizira maalum inayohusiana na masuala ya Sheria, Katiba na utawala bora  jambo ambalo ndio msingi wa ukuzaji wa uchumi wa Nchi katika nyanja zote.

Pia Rais huyo wa Chama cha mawakili alisema kuna kila sababu ya kuipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuja na sera ya dhana ya Uchumi wa Buluu na kuahidi kuwa kupitia umoja huo utaunga mkono sera hiyo kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa Nchi na maendeleo ya watu wake.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha mawaiili Zanzibar Slim Abdulla alimuleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa, kufanyika kwa mkutano huo kutasaidia kwa wanasheria wa ndani kujitathmini kupitia huduma za kisheria wanazozitoa ili kujiridhisha kama zinakidhi matakwa ya kikanda.

Umoja wa Vyama vya mawakili Afrika Mashariki umeanzishwa mnamo mwaka 1995 na unajumisha nchi zote wanachama wa Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.