Habari za Punde

Walimu Nguvu Moja na Msingi wa Maendeleo ya Tanzania.


Mkuu  wa Wilaya  Kaliua Mkoani Tabora Ndg.Paul  Chacha  akizungumza na kufungua Warsha ya Siku moja ya  mafunzo ya kuwajengea uwezo Viongozi wa Chama Wilayani humo
Katibu wa Chama Cha Walimu Wilayani Kaliua, Kessy Kidifu
Katibu wa chama cha  walimu  mkoa wa Tabora, Digna Nyaki akisitiza jambo kwa wajumbe wa chama  cha walimu wilaya ya kaliua mkoani hapa.

Baadhi ya wajumbe wa chama cha walimu wilaya ya Kaliua wakisikiliza wamaelekezo ya viongozi wao

Na.Lucas Raphael - Tabora.
Chama cha cha walimu mkoani Tabora kimeshauriwa kuwa na subira wakati Taifa linaendelea kushughulikia changamoto na madai mbalimbali  ya watumishi nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu  wa Wilaya Kaliua mkoani Tabora, Paul  Chacha  katika warsha ya siku moja ya  kuwajengea uwezo viongozi wa chama wilayani humo ilifanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Kaliua.

Alisema kwamba serikali ya awamu ya sita imedhamiria kushughulikia changamoto  mbalimbali na madai  ya watumishi nasio walimu tu bali wafanyakazi wote nchini.

Alisema kwamba serikali imeanza kulipa madai mbalimbali ya watumishi wa kada zote wakiwemo walimu pamoja ,kupandisha na kuwapandisha madaraja watumishi wake.

Alisema kwamba walimu ni hatua na nguzo ya kwanza katika maendeleo ya taifa na kwamba serikali inatambua mchango wao na  hivyo  hawana budi kutembea kifua mbele.

“Upungufu wa walimu katika shule za sekondari na msingi,  madai ya mishahara na yasiyokuwa ya mishahara yanaendelea kushughulikiwa  katika ngazi ya kitaifa  hivyo  tuwe  na subira na changamoto hizi hazipo kwa walimu pekee bali kwa watumishi  wote nchini.’’alisema mkuu wa wilaya Chacha.

“Hata hivyo, changamoto ambazo zipo ndani  ya uwezo wangu kama Mkuu wa Wilaya sitasita kuzitatua ili haki ya mtumishi na raia awaye yote wa nchi  hii aishie Wilayani  humu  ilindwe. Simu yangu iko wazi masaa  24  hivyo karibuni sana.’’ Alisisitiza.

Awali akisoma risala mbele ya Mkuu wa Wilaya , Katibu wa Chama Cha Walimu Wilayani Kaliua, Kessy Kidifu alisema chama hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa walimu, malimbikizo ya madeni yakiwemo likizo, matibabu, mapunjo ya mishahara na uhaba wa nyumba za walimu shuleni.

Alisema upungufu wa walimu katika shule za  sekondari 20 zilizopo  ni Walimu 256 na  1,544 wa shule za msingi ili  kufikia idadi  ya Walimu 3,355 wanaotakiwa wilayani Kaliua.

Aidha alisema kwamba madeni ya mishahara na yasiyokuwa ya mishahara katika shule za sekondari Wilayani Kaliua  mpaka  sasa ni shilingi 96,426,202.67 na shilingi 141,082,225 zinazohusu  matibabu  na uhamisho  katika shule za msingi. Alifafanua  katibu huyo.

Hata hivyo Katibu wa chama cha  walimu  mkoa wa Tabora, Digna Nyaki alisema kuwa mkuu wa wilaya hiyo  amewaachia walimu zoezi la kufanya ambalo ni kufundisha kwa bidii.

Sanjali na hilo aliwataka walimu kufaulisha kwa uhalali kupitia mitihani ya ndani na kitaifa  wakati serikali ikiendela  kushughulikia  madai yatokanayo na utumishi wao.

Chama cha walimu nchini Tanzania (CWT) kilisajiliwa 1/11/1993  kwa namba ya usajli TU. 002 chini ya sheria ya vyama vya  wafanyakazi (The Trade Unions Ordinance Camp No. 381 ya mwaka 1956 kabla ya sheria mpya ya bunge ya vyama vya wafanyakazi (The Trade Union Act No .10 ya mwaka 1998 ambapo mwaka 2000 chama hicho kilisajiliwa tena chini ya sheria hiyo na kupata namba ya usajili TU.004.

Ilielezwa kuwa malengo mahususi ya chama hicho ni kutetea haki za walimu hususani mishahara bora, miundo ya utumishi wa walimu, kuwaendeleza  walimu  kitaaluma na kiuchumi, kutetea na kudai miundombinu bora  kazini yakiwemo makazi bora, kusuruhisha migogoro kwenye ajira zao, kuwawezesha kutoa maoni  yao kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji na kuunganisha nguvu pamoja ili kudai haki  zitokanazo na utekelezaji wa majukumu yao kwa umma wa Watanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.