Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto yafanya mazungumzo na Shirika la Marekani linaloshughulikia Misaada ya Ukimwi Duniani (PEPFAR), ujumbe huo umekuja kufuatia ziara ya Balozi wa Marekani aliyoifanya Zanzibar hivi karibuni.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Issa Mzee - Maelezo 15/12/2021
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Shirika la Marekani linaloshughulikia Misaada ya Ukimwi (PEPFAR) ili kuhakikisha watoto wanazaliwa bila kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa wazazi wao.
Alisema kumekuwa na tatizo la maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa watoto kutoka kwa wazazi wao wakati wa kujifungua, hivyo umefika wakati wa kuhakikisha watoto wote wanazaliwa salama.
Alisema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Shirika la Marekani linaloshughulikia Misaada ya Ukimwi Duniani (PEPFAR), walipofika ofisi kwake Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo.
Mazrui alisema mpango wa serikali ni kuhakikisha mapambano dhidi ya Ukimwi yanafanikiwa, kama yalivofanyika na kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa malaria Visiwani Zanzibar.
“Tumefanikiwa kuyadhibiti malaria kwa kiwango kikubwa hivyo hivi sasa tunataka kuondoa Ukimwi kwa kiwango kikubwa nchini” alisema Waziri.
Aidha alisema kufuatia ziara ya Balozi wa Marekani aliyoifanya Zanzibar imesababisha shirika hilo kuwa tayari kufanya kazi na serikali na kuipatia misaada ili kuhakikisha mikakati ya kupambana na ukimwi inafanikiwa Nchini.
No comments:
Post a Comment