Habari za Punde

Sheikh wa Mkoa wa Tanga Amewataka Wananchi Kutokupuuza Kuchukua Tahadhari.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAUMINI wa dini ya kiislamu na wananchi wote Mkoani Tanga wametakiwa kuacha kupuuzia kuendelea kuchukua tahadhari katika kujikinga naa maambukizi dhidi ya Uviko 19 pamoja na kupata chanjo.

Wito huo umetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Tanga Jumaa Luuchu wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa bado Mataifa linasumbuliwa na ugonjwa huo hivyo ni vema sana wananchi wakaendelea kuchukua tahadhari.

"Tuna tatizo kubwa la ugonjwa huu wa Uviko 19 ambao unaoendelea kutikisa Mataifa mbalimbali, napenda niwasisitize kuchukua tahadhari kwa kutuata masharti ya wataalamu wa afya, sisi viongozi wa dini hata kwenye nyumba zetu za ibada ni kusisitiza waumini wetu kujikinga ikiwa ni pamoja na usafi" amesema.

Aidha Luuchu amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa serikali na kuonesha moyo wa uzalendo kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha pindi litakapoanza zoezi la sensa ya watu na makazi ambayo linatarajiwa kufanyika mwaka huu.

Amesema, "lakini pia mwaka huu ni mwaka wa sensa, niwahimize waumini na watu mbalimbali tujitokeze katika jambo hili pa kuhesabiwa ili kuweza kuipa serikali nafasi nzuri ya kufanya tathmini ya kuweza kujua kwamba mahitaji yetu ndani ya serikali lakini pia ni faida kwetu wananchi".

Sambamba na hayo Shehe huyo amesema Watanzania wanatakiwa kumrudia Mungu na kuomba nchi iendelee kuwa na amani na utulivu kwani viapopatikana vitu hivyo mambo mengine yote yatakuwa mepesi huku akitoa wito kwa wananchi hao kushirikiana na kushikamana katika mambo yanayoleta maendeleo.

"Jambo la kumshukuru Mungu ni kuona tumemaliza mwaka mwengine nchi yetu ikiwa na amani na utulivu, tumeanza mwaka mwengine hatuna budi kumuomba yeye atuepusha na kila shari, mimi na viongozi wenzangu wa dini kazi yetu kubwa ni kuiombea kwa Mungu nchi yetu iendelee kubaki ikiwa salama" amesisitiza Shehe Luuchu.

"Wito wangu kwa waumini na wakaazi wa Tanga kwa ujumla ni kushirikiana na kushikamana pamoja katika mambo mbalimbali mazuri ambayo yatatuletea maendeleo, bila kusahau kuwapeleka watoto shuleni wakapate elimu kwa manufaa yao ya baadae lakini pia kupata Taifa la baadae lenye wasomi" ameongeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.