Habari za Punde

Wanasiasa kuweni makini na kauli mnazotoa kwa wananchi - DK Hussein Mwinyi


 

                                       STATE HOUSE ZANZIBAR

                       OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

                                          PRESS RELEASE

 

Zanzibar                                                                        January 10, 2022

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha Wanasiasa kuwa makini na kauli wanazotoa kwa wananchi, pamoja na kuhakikisha Sera za Vyama vyao vinazingatia umuhimu wa kuwaunganisha Watanzania badala ya kuwafarakanisha.

Dk. Mwinyi ametoa ukumbusho huo katika Uzinduzi wa Kikosi Kazi cha kuchakata hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa Wadau wa Demokrasi ya Vyama Vingi, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip -  Airport Zanzibar.

Amesema masuala ya kisiasa yanagusa hisia za wananchi kwa namna mbali mbali, huku wananchi hao wakipokea matamko na kauli za wanasiasa kwa upeo na uwono tofauti, hivyo ni jukumu la wanasiasa kuwa makini na kauli wanazotoa pamoja na vitendo vyao ndani ya jamii.

Alisema wajumbe wa kikosi kazi walioteuliwa wana wajibu wa kutumia hekima, busara, uzalendo na uzoefu katika uchambuzi watakaoufanya na kuepuka hoja zitakazobainika zinaweza kuleta migongano au kuwa kikwazo cha maendeleo.

Aidha, aliwataka wajumbe hao kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kufanyakazi kwa kuzingatia maadili na kanuni zinazowaongoza kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

“Msilazimishe hoja kwa kulinda na kutetea sera na maslahi ya vyama vyenu Demokrasia itawale wakati wa kufanya maamuzi mazito ambayo mmetofautiana kimawazo na mitazamo”, alisema.

Dk. Mwinyi, alisema mchakato wa hoja hauna budi ulenge katika kuendeleza siasa zenye lengo la kuzidi kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha misingi ya usawa, umoja na mshikamano.

Aliahidi Serikali zote mbili (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika katika kutekeleza na kukamilisha majukumu ya kikosi hicho.

Alieleza kufurahishwa kwake na wajumbe walioteuliwa, wakiwemo wataalamu wabobezi katika masuala ya Uongozi, usuluhishi wa migogoro, utawala bora na haki za binadamu pamoja na masuala mbali mbali ya kisheria, huku akibainisha imani yake kuwa maamuzi yatakayopitishwa  yatakuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Aliwataka wajumbe hao kuelewa kazi waliyokabidhiwa ni yenye maslahi mapana kwa Taifa, hivyo ni vyema wakatekeleza majukumu yao kwa umahiri na umakini mkubwa ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Nae, Makamo wa Kwanza wa  Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman alisema kuundwa kwa kikosi hicho ni Uwekezaji mkubwa katika mustakbali mwema wa nchi na hivyo akawataka wananchi kuthamin hatua hiyo, sambamba na kupongeza ushirikishaji wa wajumbe kutoka makundi tofauti.

Aidha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohamed alimshukuru Rais wa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi  kwa kuliongoza Taifa kwa weledi na dhamira ya kujenga umoja na mshikamano na kutaka ari iliyoonyeshwa na viongozi hao kuteremka hadi ngazi za chini.

Dk. Khalid alipongeza uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo na kusema ana imani kubwa watakwenda kufanyakazi kwa weledi na kuzingatia maslahi mapana ya taifa.

Mapema, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Profesa Rwekaza Mukandara alitoa shukurani kwa Marais wa serikali zote mbili kwa dhamira ya kuzitafutia suluhisho changamoto mbali mbali za kisiasa zinazokabili Taifa na akatumia fursa hiyo; kutoa ahadi ya wajumbe kukubali uteuzi huo huku wakifahamu jukumu kubwa lilioko mbele yao.

Kikosi Kazi cha kuchakata  Hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa Wadau wa Demokrasia ya Siasa za Vyama vingi uliofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma, kinaundwa na Wajumbe 25, chini ya Uenyekiti wa Profesa Rwekaza Mukandara na Makamo Mwenyekiti wake Hamad Rashid Mohamed. 

  

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.