Habari za Punde

Balozi wa Tanzania Nchi India Mhe.Anisa K.Mbega Awasilisha Hati ya Utambulisho kwa Rais wa India.

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa K. Mbega amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa India Mhe. Ram Nath Kovind , Ikulu (Rashtrapati Bhavan), mjini New Delhi leo tarehe 16 Februari 2022. Baada ya kuwasilisha Hati hizo, Balozi Anisa Mbega alifanya mazungumzo na Mhe. Rais Kovind. 

Wakati wa mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Balozi Anisa Mbega aliishukuru Serikali ya India kwa misaada mbambali wanayoipatia Tanzania hususan, mikopo ya masharti nafuu katika sekta ya maji pamoja na misaada mbalimbali kama vile madawa na vifaa tiba pamoja na nafasi za mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watanzania. Aidha, alimpa Mhe. Rais Kovind salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhuhu Hassan ambapo Mhe. Rais Kovind alishukuru kwa salamu hizo.

Vilevile, Mhe. Balozi Anisa Mbega aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kudumisha mahusiano yaliyopo ya muda mrefu katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii na pia kufungua milango ya ushirikiano katika maeneo mengine. 

Rais Kovind alisifu uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na India na akasisitiza kuwa India itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye nyanja mbalimbali. Aidha, alimuhakikishia Balozi Anisa Mbega kuwa Serikali ya India ipo tayari kutoa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa wepesi na ufanisi kwa maslahi ya wananchi wa pande zote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.