Habari za Punde

Tanzania Bara, Zanzibar Kutekeleza Kwa Pamoja Anwani Za Makazi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Katibu wa Baraza la Wawakilishi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Eng. Zena Said anwani ya Ofisi ya Rais – Ikulu wakati wa kikao kazi na uzinduzi wa operesheni ya anwani za makazi, Zanzibar kilichofanyika kwenye ukumbi wa Sheikh Abdul Wakil, Zanzibar. Katikati anayeshuhudia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano naTeknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla anwani ya makazi ya ofisi hiyo wakati wa kikao kazi na uzinduzi wa operesheni ya anwani za makazi, Zanzibar kilichofanyika kwenye ukumbi wa Sheikh Abdul Wakil, Zanzibar. Kulia anayeshuhudia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano naTeknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) akimkabidhi Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya anwani ya makazi ya ofisi hiyo wakati wa kikao kazi na uzinduzi wa operesheni ya anwani za makazi, Zanzibar kilichofanyika kwenye ukumbi wa Sheikh Abdul Wakil, Zanzibar. Kulia anayeshuhudia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano naTeknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbali mbali wakati wa kikao kazi na uzinduzi wa operesheni ya anwani ya makazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Sheikh Abdul Wakil, Zanzibar. Kulia aliyeketi ni Waziri wa Habari, Mawasiliano naTeknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye

Utekelezaji Tanzania Bara wafikia 3% na Zanzibar 7%

à        Ifikapo Mwezi Mei, 2022 utekelezaji unahitajika ufike 100%

à        Anwani kupatikana kwenye programu tumizi maalum ya TEHAMA ya NaPA

à        Kutekelezwa kwa Shilingi Bilioni 28 Badala ya Shilingi Bilioni 700

à        Anwani za Makazi ni Mali ya Wananchi, Wanahusika Kutekeleza

 Na Prisca Ulomi, WHMTH, Zanzibar

 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa pamoja zinashirikiana kutekeleza mfumo wa anwani za makazi nchini kwenye mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar ili iweze kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu kwa lengo la kufanikisha zoezi la sensa ya watu inayotarajiwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu ambapo uzinduzi wa operesheni ya anwani za makazi na kikao kazi kwa ajili hiyo kimefanyika leo kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Zanzibar

 Mgeni Rasmi wa kikao kazi na uzinduzi wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa tuna viongozi katika kila ngazi, kila mmoja akifanya kazi yake vizuri hakuna mzanzibari atakosa taarifa kuhusu anwani za makazi na sensa ya watu na tumeona wataalam wetu wa ndani wametengeneza mfumo wa NaPA ambao unatupatia anwani za makazi ambapo tungetumia wataalam wa nje, Serikali ingetumia fedha nyingi sana

 Ameongeza kuwa Serikali itagawa shilingi bilioni 28 kwenye mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajiili ya utekelezaji wa anwani za makazi na ugawaji huo wa fedha hizo utazingatia ukubwa wa maeneo na mahitaji halisi ya eneo husika

  “Fedha hizi zitakuja kwenye mikoa yenu, zikatumike kwa makusudi yaliyokusudiwa na tutazifuatilia kwa karibu, naamini viongozi ni wasikivu na mtatoa ushirikiano ipasavyo ili tufanikiwe utekelezaji wa jambo hili la anwani za makazi kwa kuwa hakutakuwa na muhali kwenye jambo hili na mmefanikiwa kwenye mazoezi makubwa na hili naamini nidhamu ya matumizi ya fedha itafanyika na tukitoka hapa tukawaelimishe wananchi wetu kuhusu jambo hili na tujumuishe kwenye ajenda zetu zote” amesisitiza Mhe. Abdullah

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi), Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed wakati akimkaribisha mgeni rasmi amesema kuwa masuala haya yanahitaji ushirikiano wa pamoja na ndio maana wote tuko hapa na baada ya kikao hiki kila mmoja achukue jukumu lake la kuhakikisha anwani za makazi na sensa ya watu inakamilika ipasavyo

 “Ni lazima wananchi wajue kibao hiki kipo hapa kwa manufaa gani hivyo ni muhimu kujenga uelewa kwa wananchi ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kupatikana”, amesisitiza Mhe. Mohammed.

 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa mazoezi haya mawili ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na sensa ya watu ni mazoezi mawili tofauti ila yanayotegemeana ambapo operesheni hii imelenga kuliongezea nguvu zoezi la sensa ya watu kwa sababu ya maagizo mliyotupatia kuwa zoezi la anwani za makazi linatakiwa kuisha mwezi wa tano na la sensa litaanza mwezi wa Nane mwaka huu

 Waziri Nape ameongeza kuwa zoezi la anwani za makazi ni safari ya kuelekea Tanzania ya kidijitali kwa kuwa bila anwani za makazi Tanzania ya kidijitali haiwezakani kwa kuwa tayari dunia imeshaenda kidijitali, sisi ni sehemu ya dunia na kama tunataka kwenda kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ni lazima tutekeleze mfumo wa anwani za makazi na Zanzibar ya kidijitali inawezekana

 Amefafanua kuwa mfumo huu wa anwani za makazi ni mkataba baina ya CCM na wananchi kuwa ifikapo mwaka 2025 tuwe na awani za makazi na ni uamuzi mzuri kuwa jambo hili litekelezwe kwa miezi mitano badala ya miaka 5

 “Zoezi la sensa haliwezi kutekelezwa vizuri bila anwani za makazi, hivyo tumeona ni vema mfumo wa anwani za makazi utekelezwe kwanza ili kufanikisha utekelezji wa sensa ya watu na makazi,” amesema Waziri Nape

 Ameongeza kuwa utekelezaji wa mfumo huu wa anwani za makazi ungetekelezwa na wakandarasi ungetumia zaidi ya shilingi bilioni 700 ila Serikali itatumia shilingi bilioni 28 tu kwa kuwa mfumo huu wa operesheni ya anwani za makazi ni mali ya wananchi na utatekelezwa na wananchi wenyewe mpaka kwenye ngazi ya Serikali ya Mitaa/Shehia na utasimaimwa na watendaji wa Serikali ya Mitaa/Shehia wenyewe

 Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amour Bakari amesema kuwa Wizara hizi zenye dhamana ya Mawasiliano ikiwemo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Tanzania Bara zinawajibika kuhakikisha kuwa anwani za makazi zinatekelezwa kwa kuwa anwani za makazi zinawezesha mwananchi kupata, kupokea na kufikisha huduma au bidhaa hivyo tunapaswa kuwa na anwani za makazi kwa kuwa anwani ni nyenzo  muhimu ya mawasiliano nchini na hadi sasa jumla ya shehia 30 kati ya shehia 338 za Zanzibar zina anwani za makazi ambayo ni sawa na asilimia 7 tu.

 Katika kikao kazi hicho, wataalam wa kutoka Wizara na taasisi za SMZ waliwasilisha taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka 2022; Sensa ya Majengo; na taarifa ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ambapo kwa upande wa Tanzania Bara, mtaalam wa TEHAMA, Fredrick Apina kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari aliwasilisha kwa viongozi hao namna mfumo wa NaPA unavyofanya kazi ikiwemo ukusanyaji wa taarifa na matumizi yake kwa mwananchi katika shughuli za kiuchumi na kijamii ambapo mfumo huu unamwezesha mwananchi kupata anwani za maeneo mbali mbali na huduma zinazotolewa  mahali alipo au yaliyo jirani nae

 Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Makamisaa wa Sensa; Makatibu Tawala wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Makatibu Tawala wa Wilaya; Wakurugenzi wa Miji; Mabaraza ya Manispaa na Halamashauri za Wilaya; Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi za Serikali uliofanyika kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Zanzibar.  

                                        Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini  

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.