Habari za Punde

Maadhimisho ya wiki ya mtumiaji duniani kufanyika Machi 15

 Na Khadija Khamis – Maelezo, 09/03/2022.

Mwenyekiti wa Baraza la Kuwakilisha Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (CRC) ameitaka jamii kuyatumia mabaraza mbali mbali kwa kutoa malalamiko yao katika utumiaji wa huduma  ili kupatiwa utetezi.

Amesema Baraza hilo limeundwa  kwa ajili ya kulinda kutetea kuhamasisha na kutoa ushauri kwa watumiaji wa huduma za maji nishati pamoja na gesi.

Akiyasema hayo katika Ukumbi wa Mamlaka ya Huduma ya Maji na Nishati (ZURA )wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusiana na kulinda na kutetea, maslahi ya mtumiaji wa huduma ya maji na umeme ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za maadhimisho ya wiki ya mtumiaji duniani ambayo hufanyika kila ifikapo machi 15 ya kila mwaka.

Aidha alisema kuwa baraza linafanyakazi na mtumiaji  kwa njia tofauti kwa mashirikiana ikiwemo kutoa taarifa muhimu za mtumiaji pamoja na kufuatia malalamiko katika mamlaka husika ili kupatiwa ufumbuzi wa haraka  .

Nae Afisa Elimu Mtatuzi Malalamiko (CRC) Khamis Ame Mnubi alisema kilele cha haki ya mtumiaji kitaadhimishwa kwa mfumo wa maonyesho ambayo yataanza tarehe 12 mwezi huu.

alifahamisha kuwa kutakuwa na  maonyesho ya mabaraza mbali mbali kwa ajili ya kutoa huduma kwa watumiaji ikiwemo kuwapa elimu  pamoja na kupokea malalamiko na ushauri.

Kwa upande wa Msaidizi wa Afisa Elimu na Muhamasishaji Rahma Hassan Thabit alisema jukumu la baraza ni kupokea malalamiko ya watumiaji wa huduma iwapo kumekuwa na huduma mbovu zinazotolewa na kuzifanyia kazi kwenye mamlaka husika ikiwa mamlaka ya maji au umeme.

Alifahamisha kwamba kila mtumiaji wa huduma hizo ana haki ya kuzichangia kwa utaratibu wa mtoa huduma unavyoelekeza ikipo anapata huduma.

Akitoa wito kwa watumiaji huduma hizo kuwa makini katika utumiaji wa huduma ya maji na umeme pamoja na kutoa taarifa ya matatizo yanapojitokeza.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Sheikhe Idriss Abdulwakil, Kikwajuni na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni Usawa katika Huduma za Fedha Kidigitali  (Fair Digital  Finance).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.