Habari za Punde

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni Fursa Inayohitaji Uelewa

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akisalimiana na Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot  alipofika Ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza na Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot  alipofika Ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo.


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini kunafungua zaidi milango ya kukuza mahusiano ya                kidiplomasia na fursa za kuwaletea maendeleo wananchi.                                                                       

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa akiongea na Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania, Didier Chassot, aliyefika kwa ajili ya mazungumzo na kubadilishana mawazo juu ya kuendeleza hatua mbali mbali za kusaidia maendeleo ya Nchi.

Amesema kuwepo kwa mfumo wa kuendesha Serikali kwa mashirikiano, ni fursa muhimu ya kuhamasisha mahusiano mema yanayolenga kuandaa mazingira bora ya kusaidia, na ambayo yanahitaji kujengewa misingi imara, ikiwemo ya kukuza uelewa kwa umma.

Mheshimiwa Othman ameipongeza Switzerland kwa kuwa mstari wa mbele katika kujenga ufanisi wa kisekta hapa nchini, na mfano bora katika utekelezaji wa kweli wa dhana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa duniani.

Aidha, Mheshimiwa Othman amebainisha haja ya uelewa wa umma juu ya dhana halisi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hasa kwa nchi kama Zanzibar, ambapo wapo miongoni mwa watu, wakiwemo baadhi ya viongozi wanaopinga uwepo wake.

Hivyo amesema ni vyema kujenga uelewa mpana kwa wote, kwani hata baadhi ya wanaopendelea muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hawaelewi kwanini wamekuwa na mtazamo huo. 

Kwa upande wake Balozi Chassot ameeleza azma ya Nchi yake kurudi kusaidia maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba, baada ya kushuhudia azma ya kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa dhamira ya kuungamkono juhudi za kuleta ufanisi katika sekta mbali mbali.

Ametaja sekta hizo kuwa ni pamoja na kuwawezesha wananchi kupitia misaada kwa asasi za kiraia, mfumo wa kisasa wa bima ya afya, utafiti, na kusaidia juhudi za kuzuia na kupambana na rushwa.

Katika ujumbe wake Balozi Chassot ameambatana na Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Switzerland nchini Tanzania Anayehusika na Mambo ya Kisiasa, Bi Leonor Bottaro.      

Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

24/03/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.