Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othmann Masoud Othman akielekea katika jukwaa maalum lililoandaliwa wakati wa hafla ya Maadhimishi ya Siku ya Utawi wa Jamii (kulia ) Mkuu wa Mkoa wa Majini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana na (kushoto) Waziri wa Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili Sekta ya Ustawi wa Jamii nchini, ambayo ni suala lililoamriwa na Katiba, ni wajibu wa kila mtu kujenga utamaduni wa kupenda kufanyakazi kwa moyo wa uzalendo na kuzingatia fursa, ili kufanikisha maendeleo ya kweli.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika Maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii, ambayo yamefanyika katika Viwanja vya Kariakoo, Mkoa wa Mjini Magharibi, kisiwani Unguja.
Amesema kuwa Kifungu cha 10 cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, kinaeleza maamuru muhimu ambayo inatakiwa kuyafuata ili kulinda na kuendeleza ustawi wa Jamii, kwa madhumuni ya kujenga umoja, maendeleo ya watu na wajibu wa Serikali katika kuchukua hatua kadhaa zilizoelezwa, ambazo ni pamoja na kuhakikisha kwamba msaada unatolewa kwa wale wasiojiweza, wazee, wagonjwa, watoto na wenye ulemavu.
Aidha Mheshimiwa Othman ameeleza kwamba kipimo cha nchi au taifa lolote linalojali maendeleo ya kweli, ni pamoja na kuangalia mafanikio yake katika kujenga ustawi bora wa jamii, na wala si vinginevyo.
Hivyo amehamasisha haja ya kuitumia Siku hii ya Kimataifa ya Ustawi wa Jamii, kuhakikisha umma unapima na kuwashajihisha wanaustawi kila mmoja kutekeleza wajibu wake, kwa maslahi ya maendeleo ya Nchi na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman ameeleza pia wajibu kwa vijana wote kupenda kujishughulisha na harakati mbali mbali halali, za heshima na zinazostahiki, ili kuondokana na matatizo yatakayowapelekea kupoteza mwelekeo wa maisha yao ya baadae, huku akitoa wito kwa Maafisa, Wazee, Wanawake, Watoto na wadau wote kushirikiana na kuunganisha nguvu za pamoja baina yao, jumuiya na taasisi zote, katika kupambana na matatizo ya udhalilishaji, akisema ZANZIBAR bila udhalilishaji inawezekana.
Akitilia mkazo suala la udhalilishaji wa kijinsia katika jamii Mheshimiwa Othman amesema, “nataka niwahakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Nane itaendelea kuwa mstari wa mbele kupinga udhalilishaji, ambapo mnaelewa kazi imeanza ikiwemo kuanzishwa kwa Mahakama maalum ya kupambana na vitendo hivyo”.
Mheshimiwa Othman ameipongeza Idara ya Ustawi wa Jamii kwa kufanikisha Maadhimisho ya Mwaka huu kwa ufanisi mkubwa, ambayo yanabeba Kauli Mbiu isemayo, “Co-building a New Eco-Social World: Leaving no one Behind”, ambapo maana yake ni ‘Kujenga kwa Pamoja Dunia yenye Mazingira ya Ustawi wa Jamii: Bila ya Kumuacha Mtu yeyote Nyuma’.
Katika wito wake Mheshimiwa Othman amesema kuwa ni wajibu kwa wanafanyakazi katika maeneo tofauti yakiwemo Hospitali, Vituo vya Kulelea na Kutetea Haki za Wazee na Watoto, Mahakamani, Vyuo Vikuu, Polisi, Magereza, Maskulini, na Asasi za Kiraia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kama inavyostahiki, huku akisisitiza kwamba ni dhima ya kila mmoja kujenga na kuendeleza misingi ya ustawi wa jamii kwa kadri inavyowezekana kuanzia ngazi ya familia.
Naye, Waziri wa Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, amesema kuwa Maadhimisho hayo yanayofanyika Jumanne ya Tatu (3) ya Mwezi wa Machi ya kila mwaka, pamoja na mambo mengine, yanalenga katika kutambua na kutathmini juhudi na michango inayotolewa na Maafisa na Wadau wote wa Ustawi Jamii, ili kufanikisha utoaji wa huduma, misaada, maendeleo ya Nchi, na Taifa kwa ujumla.
Mbali na kaulimbiu yake, kila mwaka Siku hii hubeba ujumbe mahsusi, ambapo kwa mara hii unasema, “kufanya kazi kwa pamoja, kutoa huduma bora za ustawi dhidi ya ukatili na udhalilishaji”, kutokana na azma iliyotajwa ya kuhamasisha umuhimu wa mahusiano ya kijamii katika kupinga ukatili na udhalilishaji, kwa wanajamii wote.
Viongozi mbali mbali wamehudhuria katika hafla hiyo wakiwemo Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mheshimiwa Omar Said Shaaban, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mheshimiwa Suleiman Masoud Makame,Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi – Unguja, Bw. Idrisa Kitwana Mustafa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bi Abeida Rashid Abdalla, na Watendaji kutoka Asasi za Kiraia, ndani na nje ya Zanzibar.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais waZanzibar
15/03/2022.
No comments:
Post a Comment