Habari za Punde

Profesa Ndalichako Amshukuru Rais kwa kutoa fedha za Maendeleo ya Jimboni

Mbunge wa Jimbo la Kasulu mjini mkoani Kigoma Profesa Joyce Ndalichako, amemtumia Rais Samia Suluhu Hassan, Salaam za Pasaka na shukurani kwa uwezeshaji mkubwa wa kifedha unaowezesha kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati katika jimbao lake na wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Katika Salaam hizo, Profesa Ndalichako amebainisha kuwa, Halmashauri ya mji wa Kasulu katika Jimbo la uchaguzi la Kasulu Mjini inatarajia kufungua shule mpya mbili za sekondari ifikapo 2023 kufuatia serikali ya Mama Samia kutoa fedha za kutosha kutekeleza miradi hiyo sambamba juhudi za Mbunge wa jimbo hilo Profesa Joyce Ndalichako kuhakikisha kila kata inakuwa na shule yake ya Sekondari

Akikagua ujenzi wa shule za sekondari katika kata za Mwilamvya na Kimobwa mjini Kasulu, Profesa Ndalichako amebainisha kuwa chini ya mpango wa maendeleo serikali ya Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha takribani bilioni moja kukamilisha ujenzi wa shule za Milamvya na Kimobwa ili zipokee wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023

“Tayari tumeshaleta kiasi cha shilingi milioni 470 kwa kila kata kwa ajili ya ujenzi unaoendelea, na ninaridhishwa na hatua mbalimbali za ujenzi huu, na niwaahidi kwamba nitaendelea kutafuta fedha ili shule hizi zianze kupokea wanafunzi mwakani, tayari sh. Milioni 130 nyingine zinatarajiwa kuwasili jimboni kwa ajili ya shule hizi, kinachotakiwa na kuongeza kasi ya ujenzi kwa fedha zilizopo ili kuruhusu pesa nyingine kuletwa”. Alibainisha Ndalichako

Profesa Ndalichako amebainisha kuwa, kupatikana kwa pesa hizo kunatokana na kiu ya wananchi wa Kasulu mjini na ushirikiano mzuri uliopo baina ya wabunge na madiwani na ameahidi kuwa yeye binafsi ataendelea kufanya ushawishi kwa wadau wa maendeleo na kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano mama Samia ili pesa Zaidi zipatikane kwa ajiili ya miradi ya maendeleo katika jimbo la Kasulu.

“Ninamshukuru sana na kumpongeza mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyochapa kazi na kukubali maombi ya wabunge nikiwemo mimi na hatimaye kutoa fedha kwa ajii ya maendeleo ya sekta mbalimbali mkoani Kigoma, Mama yetu anatupenda sana na ninachukua fursa ya hadhila hii kumshukuruu sana Rais wetu, Anaupigwa mwingi kwakweli na kazi inaendelea” Alisisitiza Mheshimiwa Profesa Ndalichako akiongea na wananchi katika kata za Kimobwa na Mwilamvya

Aliongeza kuwa, kupitia katika mipango mbalimbali Jimbo la Kasulu mjini limefanikiwa kujenga kituo kipya cha afya katika kata ya Nyansha pamoja na kata ya Heru juu ambacho ujenzi wake umeanza baada ya kupokea fedha kutoka serikali kuu.

Aidha Profesa Ndalichako amebainisha kuwa, kutokana na ushawishi wa ofisi yake pamoja na kukubalika kwa maombi ya wananchi wa Kasulu, zahanati tatu katika kata za Kumnyika na Mwilamvya zimejengwa na nyingine mpya mbili zimeanza kujengwa katika mitaa ya Murusi na Nyumbigwa.

Diwani wa Kata za Mwilamvya Bw. Emmanuel Gamuye pamoja na Gilbert Moshi wa kata ya Kimobwa wamemshukuru Mbunge wao kwa kuwapa ushirikiano na kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradii ya maendeleo katika Kata zao na kumwahidi ushirikiano zaidi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmshauri ya Mji wa Kasulu Bw. Noeli Hanura amepongeza uchapakazi wa Profesa Ndalichako na kuongeza kuwa wao kama halmashauri wanamuunga mkono Mbunge pamoja na Rais Samia kwa kuendelea kuchapa kazi ili malengo yaliyowekwa yatimie.

Mheshimiwa Hanura anataja kuwa moja ya mambo ambayo yanampa faraja ni ujenzi wa kituo cha afya katika kata yake ya Heru juu ambao kwa miaka mingi ulishindikana licha ya kuwa katika miango ya maendeleo kwamba kuanza kwa ujenzi huo ni fahari kwa wananchi wa kata hiyo na jimbo la Kasulu kwa ujumla, huku akimpongeza mbunge kwa kukipambania kituo hicho cha afya.

Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni Mbunge wa Kasulu mjini na pia Waziri wan chi Ofisi ya Waziri mkuu, Vijana, ajira na wenye ulemavu yupo mjini Kasulu kwa mapumziko ya Pasaka pamoja na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo lake la uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.