Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe Polepole Ikulu Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe.Humphrey Polepole alikpofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, mazungumzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 28-4-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe.Humphrey H.Polepole (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo kwa mazungumzo na kujitambulisha mazungumzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemueleza Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi Humphrey Hezron Polepole umuhimu wa kwenda kuifanyia kazi na kuipa kipaumbele Sera ya Diplomasia ya Uchumi nchini humo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi Humphrey Hezron Polepole ambaye amefika Ikulu kwa ajili ya kuaga akiwa tayari kuelekea katika kituo chake kipya cha kazi nchini Malawi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Polepole kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelekeza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi na nchi za nje ambayo ndio Dira  yake katika mashirikiano na nchi hizo kiuchumi hivi sasa.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa kiongozi huyo kwenda kuifanyia kazi Sera ya Diplomasia ya Uchumi nchini  Malawi hasa katika sekta ya biashara.

Kwa upande wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Polepole kwamba Zanzibar ina mazao mengi yanayotokana na bahari ambayo ni bidhaa muhimu katika biashara nje ya nchi likiwemo dagaa ambalo bado halijapata soko nchini Malawi.

Aliongeza kuwa, kwa hivi sasa biashara ya dagaa linalotoka Zanzibar imekuwa ikifanyika zaidi katika nchi ya Jamhuri ya Congo na kuimarika kwa kiasi kikubwa  hivyo, ni vyema fursa hiyo ya kibiashara ikatumika katika nchini Malawi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba mbali na suala la kiuchumi na kibiashara Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishiriki vyema katika kupigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika ikiwemo Malawi hivyo, ni vyema uhusiano na ushirikiano wa kimipaka ukaendelezwa hasa kwa vile nchi hizo zimepakana.

Alisisitiza kwamba ushirikiano wa mipaka ukiimarika kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Malawi utaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kupambana na kukinga vitendo viovu vya kiulinzi na kiusalama sanjari na kulinda mipaka kati ya nchini mbili hizo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Balozi Pole pole kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi na kumhakikishia kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itampa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza jukumu lake hilo jipya.

Nae Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi Humphrey Hezron Polepole alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba atayafanyia kazi maelekezo yote aliyompa kwa kutambua kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Polepole alisema kuwa kwa vile Zanzibar hivi sasa imejikita kuweka mikakati yake katika kuimarisha uchumi wa buluu atahakikisha Sera hiyo anaifanyia kazi kwa kutafuta  fursa hasa zile za biashara zinazotokana na rasilimali za bahari ikiwemo bidhaa ya dagaa katika soko la Malawi.

Pamoja na hayo, Balozi Polepole alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza na kuukuza uchumi wa Zanzibar hasa katika mikakati yake ya Sera ya uchumi wa buluu ambayo aliahidi na yeye kwa upande wake kwenda kuifanyia kazi nchini Malawi.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.