Habari za Punde

Waziri Mhe Harusi Said Ziarani Kisiwani Pemba.

 

Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bi Farhat A. Mbarouk akiimuelezea Waziri wa  nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na ujumbe alioongozana nao kuhusu  mradi wa ujenzi wa Ukuta wa mawe katika fukwe ya mwambao wa eneo la Msuka mara baada ya kuukagua ukuta huo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mh Harusi Said Suleiman akiwa ameongozana na Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bi Farhat A. Mbarouk na watendaji wa idara hio kukaguwa maendeleo ya mradi wa ujenzi wa mabwawa ya maji machafu ulipo Kichungwani Pemba 

Na Raya Hamad ….OMKR

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mh Harusi Said Suleiman amewataka watendaji wa ofisi hiyo kujitathmini na kujipanga upya katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ili lengo la serikali la utoaji wa huduma bora kwa wananchi liweze kufikiwa kwa wakati.

Mh. Harusi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa Idara, Tume na Mamlaka zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika mkutano wa kujitambulisha kufuatia uteuzi wake hivin karibuni ili kuona maendeleo ya taasisi hizo kwenye ukumbi wa mkutano Gombani Chake Chake.

Amesema ni wajibu wake watendaji na wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na kufuata muongozo wa utumishi ambapo pamoja na kujitathmini kiutendaji, kuona kipi ambacho amekifanikisha kwa muda wa wiki nzima ambacho kimeweza kuleta tija kwa taasisi na wananchi.

Aidha Mh. Harusi amewaambia watendaji hao kuzidisha ari na nguvu ya kiutendaji kwa wananchi wanaohitaji huduma na kutatua changamoto zao ukizingatia kuwa sekta za ofisi hii ni mtambuka hivyo hawapaswi kukaa ofisini bali wajitoe kufikisha elimu na huduma stahiki kwa wanajamii.

“watendaji hakikisheni mnashirikiana pamoja ili wale wanaokufateni mnaowangoza nao waone kuwa viongozi wao wapo makini na hakutakuwa na mwanya wa kufanya yaliyo sio bali kama zipo changamoto zigeuke kuwa fursa kwa kuwa wabunifu wa mipango mipya yenye kuleta tija “alisisitiza Bi Harusi

Mapema Mhe Harusi alionana na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mattar Zahor Masoud na kufanya mazungumzao mafupi ofisini kwake ambapo viongozi hao wote wameahidi kushirikiana pamoja ili kufanikisha majukumu yatayoleta mafanikio ndani ya mkoa huo kwa vile masuala yanaosimamiwa na ofisi hio yanamgusa kila mtu.

Afisa Mdhamini wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bw Ahmeid Abubakar amemuahidi Waziri Bi Harusi kwa kushirikiana na watendaji wanahakikisha wanatekeleza majukumu yao vyema kusimamia miradi ya maendeleo na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi

Mh.Harusi amezitembelea Idara na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Kudhibiti  na Kupambana na Dawa za Kulevya, Baraza la Watu wenye Ulemavu na Tume ya UKIMWI pia ameikaguwa miradi ya maendeleo ukiwemo Mradi wa ujenzi wa tuta la kuzuwia maji ya chumvi yasiingie katika mashamba uliopo Tovini

Kwengine ni kuona mradi wa ujenzi wa Ukuta wa mawe katika fukwe ya mwambao wa eneo la Msuka, mradi wa ujenzi wa mabwawa ya maji machafu ulipo Kichungwani, pamoja na kufika Likoni Kojani kuangalia eneo linalotarajiwa kujengwa ukuta wa kuzuwia mmongonyoko wa fukwe ambao pia utaunusuru mbuyu wa asili uliopo eneo hilo ambao kwa sasa upo hatarini kuanguka

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.