Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe. Chillo Ataka Elimu Matumizi ya Ardhi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Khamis Hamza Chillo akizungumza wakati wa mkutano wa Mawaziri wa Wizara za Kisekta na viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 mkoani humo.

Na Munir Shemweta, WANMM KILIMANKARO

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Khamis Hamza Chillo amewataka viongozi wa mkoa na wilaya nchini kuhakikisha wanawaelimisha wananchi namna bora ya matumizi ya ardhi.

 

Chillo alitoa kauli hiyo April 30, 2022 wakati wa mkutano wa Mawaziri wa Wizara za Kisekta na viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kupeleka mrejesho wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

 

"Twendeni tukawaambie watu namna bora ya utumiaji au matumizi bora ya ardhi, ardhi hizi tunaziumiza kuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika ardhi mwisho wa siku tunaiharibu ardhi" alisema Chillo

 

Aliwataka viongozi hao wa mkoa na wilaya kwenda kuwafahamisha wananchi namna ya kufanya shughuli za kibinadamu bila kuchafua mazingira au kuharibu ardhi.

 

"Kuna shughuli nyingi za kibinadamu zinafanyika kama vile ujenzi wa makazi usiozingatia taratibu na mwisho wa siku ardhi inaharibika na pale inapoharibika basi na mazingira nayo hayatakuwa salama" alisema Naibu Waziri Chillo.

 

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta Dkt Angeline Mabula alieleza kuwa ni jukumu la viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji kuhakikisha wanalinda maeneo yote ya hifadhi kwa lengo la kuepuka uharibifu unaoweza kutokea.

 

Akigeukia utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 nchini, Dkt Mabula alisema kwa mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na migogoro kwenye vijiji 12 ambapo kati ya vijiji hivyo vijiji 8 Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuendelea kubaki kwenye maeneo yake huku vijiji 4 vikitakuwa kufanyiwa tathmini.

 

"Kati ya vijiji 12 vilivyoingia kwenye migogoro ya matumizi ya ardhi na maeneo ya hifadhi hapa Kilimanjaro vijiji 8 mhe rais ameridhia vibaki.  Si jambo jepesi watu kuvunja sheria na kutakiwa kubaki, nisisitize watu wasiendelee kuvunja sheria na kusubiri huruma ya rais" alisema Dkt Mabula.

 

Timu ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta bado inaendelea na ziara zake katika mikoa mbalimbali nchini kupeleka mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa  migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 ambapo katika awamu hii ya pili timu ya Mawaziri hao imetembelea mikoa ya Pwani, Tanga, Morogoro, Mara na Arusha

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.