Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.,Hussein Ali Mwinyi Ametoa Salamu za Pole kwa Wanafunzi Pamoja na Walimu wa Skuli ya Ufundi Kengeja Pemba.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za pole kwa wanafunzi pamoja na walimu wa skuli ya Sekondari ya Kengeja Ufundi kiswani Pemba kufuatia kuungua moto kwa daghalia ya wanawake katika skuli hiyo.

Katika salamu hizo za pole, Rais Dk. Mwinyi alieleza jinsi alivyopokea kwa mshituko na huzuni kubwa tukio hilo lililotokea hapo jana lililosababisha uharibifu wa jengo hilo, vitanda, vifaa vya kusomea vya wanafunzi pamoja na vifaa vyengine vya matumzi ya wanafunzi.

Salamu hizo za pole zilieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha inawawekea mazingira mazuri mbadala kwa wakati huu wanafunzi hao pamoja na kuhakikisha hali ya daghalia hiyo inarejea kama ilivyokuwa mwanzo ili waweze kuendelea na masomo yao kama kawaida.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzitaka taasisi husika kufanya uchunguzi wa kina juu ya ajali hiyo ya moto ili majanga kama hayo yasiendelee kutokea kwa mara nyengine tena hasa ikizingatiwa kwamba tayari matukio kama hayo yamesharipotiwa hivi karibuni katika skuli ya Utaani na Madungu kisiwani humo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud viashiria vya mwanzo vya tukio hilo la moto vinaonesha kwamba  linatokea na hitilafu ya umeme lakini hakuna mwanafunzi aliyepata majeraha ya moto huo na wanafunzi wote wako salama.

Alisema kuwa athari zaidi imetokea kwa kuungua jengo pamoja na vifaa vyote vya wanafunzi vilivyokuwemo ndani huku akisema kwamba Serikali ya Mkoa inaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo sambamba kuwasilisha  misaada mbali mbali kwa ajili ya wanafunzi hao ili waweze kuendelea na masomo yao ipasavyo.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.