Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameupongeza Mkufo wa Fedha wa Dunia "Global Fund"

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mkuu wa Idara ya Afrika Mfuko wa “Global Fund” kutoka Geneva Bw.Linden Morrison, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo akiwa na ujumbe wake Dr.Sarah Asiimwe na Dr. Patrick Githendu, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 10-6-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein  Ali Mwinyi akizungumza na Mkuu wa Idara ya Afrika Mfuko wa “Global Fund” kutoka Geneva Bw. Linden Morrison, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 10-6-2022, akiongozana na ujumbe wake

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mkuu wa Idara ya Afrika Mfuko wa “Global Fund” kutoka Geneva Bw. Linden Morrison, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 10-6-2022, akiwa na ujumbe wake

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza Mfuko wa Fedha wa Dunia (Global Fund), kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimaisha sekta ya afya hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Afrika kutoka Mfuko wa Fedha wa Dunia (Global Fund), Linden Morrison kutoka Geneva Switzerland, akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Mfuko huo umekuwa ukitoa msaada wake mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya afya ikiwemo changamoto ya UVIKO-19 kwa kipindi chote.

Alieleza kuwa mbali ya hatua hiyo Mfuko huo wa Fedha wa Dunia (Global Fund), umeweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa miradi mbali ambali ukiwemo ujenzi wa miradi ya hospitali za Wilaya na Mkoa unaotokana na fedha za UVIKO-19.

Rais Dk. Mwinyi alifafanua hatua zilizofikiwa hivi sasa katika matumizi ya fedha hizo ambapo alifahamisha kwamba kiasi kikubwa cha fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya hospitali za Wilaya na Mkoa Unguja na Pemba.

Aliufahamisha Ujumbe huo kwamba kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya kwa kuondoa na kupunguza msongamano katika hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambapo hivi sasa wagonjwa wengi wanaitegemea hospitali hiyo kwa kesi za rufaa na zisizo za rufaa.

Alisisitiza kwamba ujenzi huo utahusisha malengo ya Serikali ya kuweka mifumo na taratibu bora za kinga na tiba pamoja na utoaji wa huduma nzuri kwa wananchi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza matarajio yake kwamba Mfuko huo utaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika hatua zinazofuata za kuendeleza hospitali hizo mpya kwa upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa kada mbali mbali.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Mfuko huo kwa ushirikiano wake uliouonesha katika kupambana na maradhi ya Malaria hapa Zanzibar ambapo mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano barani Afrika yameweza kupatikana.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushirikiana na sekta binafsi katika uendeshwaji wa vitengo vya uchunguzi wa maradhi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba.

Nae Mkuu wa Idara ya Afrika kutoka Mfuko wa Fedha wa Dunia (Global Fund), Linden Morrison alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa matumizi mazuri ya fedha za UVIKO-19 hasa katika ujenzi wa miundombinu ya hospitali unaoendelea.

Katika mazungumzo yake, kiongozi huyo kutoka Makamo Makuu ya Mfuko huo Mjini Geneva, alisema kwamba mafanikio hayo yaliyopatikana katika matumizi ya fedha za UVIKO-19 ni ya kupigiwa mfano nje na ndani ya bara la Afrika.

Hivyo, alieleza utayari wa Mfuko huo wa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uendelezaji na utoaji wa huduma katika hospitali hizo mpya zinazoendelea na ujenzi hivi sasa.

Alieleza kuvutiwa na dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushirikiana na sekta binafsi katika uendeshaji na utoaji huduma katika baadhi ya maeneo huku akiahidi kwamba Mfuko huo utaunga mkono utekelezaji wa mpago huo.

Aidha, Mkuu huyo kutoka Idara ya Afrika kutoka Mfuko wa Dunia (Global Fund), Linden Morrison aliahidi kwamba Mfuko huo uko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa wataalamu pamoja na mafunzo yanayohitajika.

Pamoja na hayo, aliisifu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake za kuendesha program mbali mbali kwa kushirikiana na Mfuko huo na kuweza kupata mafanikio katika maradhi ya Malaria.

Alifahamisha kwamba Mfuko huo utaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutegemea mahitaji yaliyopangwa.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.