Habari za Punde

Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe,.Hemed Suleiman Abdulla Kutembelea Ujenzi wa Miradi katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo 16-6-2022.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah akitoa maagizo kwa watendaji wa Shirika la Bandari Zanzibar na kuwataka kuhakikisha wanasimamia zoezi la upakuaji na upakiaji wa makontena yanayoingia kupitia Bandari ya Malindi alipofanya ziara Bandarini hapo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kuhusu ujenzi wa soko la Mwanakwerekwe alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa soko hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa eneo linalojengwa maduka Darajani Mjini Unguja akizungumza na Viongozi mbali mbali katika ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa Masoko Mkoa wa Mjini Magharibi na kueleza imani yake kwa kampuni ya Africab iliyopewa ujenzi wa Darajani Bazaar ambao utakamilika hivi karibuni.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Muhamed akizungumza katika ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ya kukagua mradi ya masoko inayojengwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikagua na kujionea ujenzi wa Maduka ya Darajani (Darajani Bazaar) unaojengwa na kampuni ya Africab ambapo ameridhishwa na ujenzi huo unavyoendelea.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa muda wa wiki mbili kuitaka Wizara ya Nchini Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kukaa na Muwekezaji aliekabidhiwa Ujenzi wa Soko la Jumbi na Mwanakwerekwe na kufuata                taratibu za kisheria ili kuendelea na ujenzi wa masoko hayo.                                                            

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa Miradi ya Masoko katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameeleza kuwa hatua iliyofikia katika masoko hayo sio ya kuridhisha jambo ambalo haliendani na azma ya Serikali ya Awamu ya Nane kwa kushirikiana na Wawekezaji wa ndani na wa nje katika kujenga miradi mbali mbali ya maendeleo.

Ameeleza kuwa Serikali itaangalia namna bora ya kujenga soko la Jumbi ili kuwasaidia wananchi na wajasiriamali kuweza kupata eneo zuri na la kisasa ambalo wataweza kujipatia huduma zao za kila siku.

Ameeleza kuwa Serikali imeelekeza Imani yake kwa Sekta Binafsi kushirikiana na Serikali kwa kupanua wigo katika kuijenga Zanzibar bora ambayo wananchi wake wataweza kufaidika na maendeleo.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  amemueleza mkandarasi wa Soko la Mwanakwerekwe ambae ndie anaejenga soko la jumbi kueleza changamoto zinazomkabili ili kuendana na kasi ya mkataba wa Ujenzi wa masoko hayo.

Nae waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Muhamed ameeleza kuwa Wizara hairidhishwi kuona wawekezaji kuenda kinyume na makubaliano waliyofunga katika Mkataba jambo ambalo linapelekea kuchelewa ujenzi wa Miradi hiyo.

Aidha Mhe. Masoud ameeleza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi haitomvumilia muwekezaji na Mkandarasi yoyote atakaejaribu kukiuka mikataba waliofunga na Wizara.

Katika Ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametembelea ujenzi wa Darajani Bazaar (Soko la Darajani) na kueleza kuridhishwa kwake kwa hatua iliyofikia ambapo ameeleza kuwa kukamilika kwa soko hilo kutasaidia kukuza uchumi wa Nchi na kuwasaidia wananchi kujipatia kipato.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed ametembelea Bandari ya Malindi na kujionea hali ya ushushaji na upakiaji wa Makontena na kuuahidi uongozi wa Shirika la Bandari la Zanzibar kuhakikisha wanaweka mazingira ya kupunguza mrundikano wa Makontena kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuyapeleka Makontena eneo la Bwanani ili kurahisisha ushushaji wa Makontena kwa wakati eneo la Bandari.

Aidha Mhe. Hemed amefurahishwa kuona maamuzi ya Shirika la Bandari kuweka One Stop Centre ya Shughuli za Bandari na kuwataka kuharakisha kukamilika kwa Mfumo wa kuendesha Kituo hicho na kueleza kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia ukusanyaji wa mapato na kukuza uchumi wanchi.

Pia makamu wa pili wa rais wa Zanzibar amesemakuwepo kwa one stop center eneo la bandarini kutawapunguzia wafanya biashara usumbufu wa kuhangaika kila sehem kwa ajili ya kufanya malipo na kuwarahisishia wafanyakazi wa bandari kujua idadi ya Kontena zinazoingia na zinazotoka pamoja na kudhibiti mianya ya rushwa katika eneo hilo.

Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni ahadi aliyoiiweka katika ziara yake ya Tarehe 14 Mei mwaka huu ambapo aliahidi kufatilia ujenzi huo ndani ya mwezi mmoja.

Hivyo Makamu wa Pili wa Rais ametembelea ujenzi wa Soko la Jumbi, Soko la Mwanakwerekwe, Soko la Darajani (DARAJANI BAZAAR) pamoja na Bandari ya kushushia na kupakia Makontena Malindi.

Abdulrahim Khamis - Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 16/06/2022


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.