Habari za Punde

Dk.Mwinyi Amemsimamisha kazi Mkandarasi wa Kampuni ya Associated Investment Company Ltd ya Tanzania inayojenga skuli ya Sekondari ya Mtopepo Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kumsimamisha Kazi Mkandarasi wa Kampuni ya Associated Investment Ltd ya Tanzania kwa kuchelewesha ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Mtopepo Wilaya ya Magharibi "A"Unguja inayojengwa kwa Fedha za Covid -19.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemsimamisha kazi Mkandarasi wa Kampuni ya Associated Investment Company Ltd ya Tanzania inayojenga skuli ya Sekondari ya Mtopepo Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi amechukua hatua hiyo baada ya kuona uwezo mdogo wa ujenzi unaoendeshwa na Kampuni hiyo ya Associated Investment Company Ltd ya Dar es Salaam  kwa kukengeuka mashari ya ujenzi na hivyo, kuona haja ya kuvunja mkataba wa ujenzi na Kampuni hiyo.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Kampuni hiyo tayari imeshachukua muda wa miezi sita lakini bado haijafikia hatua za ujenzi kama ilivyokubaliana na Serikali na kushangazwa kuomba miezi mengine sita.

Alisema kuwa Kampuni hiyo haifai kufanya kazi kwani haina sifa huku akishangwazwa na Mshauri Elekezi, Kampuni ya “Edge Consultacy Company” kushindwa kuishauri Serikali jinsi ya utendaji kazi mbovu wa Kampuni hiyo na kueleza kwamba Kampuni zote hizo hazina sifa wala uwezo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba ujenzi wa mradi huo umefikia hatua hiyo kutokana na Wizara husika ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutokuwa na muhali katika kusimamia miradi ya Serikali.

Hata hivyi, Rais Dk. Mwinyi alitioa maelekezo kwamba Mkandarasi huyo asipewe mradi mwengine wa aina yoyote kwani hana sifa wala vigezo.

“Kampuni haina uwezo, Kampuni haina bondi na Wizara ya Elimu ndio mmetufikisha hapa na hii ndio inatokana na yale maneno yanayosemwa kwamba Rais kasema apewe kazi.....huyu hafai”, alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuchukua hatua kwa kampuni iliyopewa kazi pale inapoonekana utekelezaji wa miradi ya maendeleo haiendi kama ilivyokusudiwa.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi, walimu pamoja na wanafunzi wa skuli hiyo mpya ya Sekondari ya Mtopepo kwamba Serikali itahakikisha inafanya juhudi za makusudi ili wakati wa sherehe za Mapinduzi za Januari 12, mwakani skuli hiyo inafunguliwa.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanziar ni kupunguza idadi ya wanafunzi wengi madarasani na ndio maana hatua za makusudi zinachukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa na kuwataka walimu na wanafunzi kuwa na subira.

Mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Soko la Wajasiriamali linalojengwa kwa fedha za UVIKO-19 huko Shehia ya Munduli, Rais Dk. Mwinyi aliiitaka Idara ya Manispaa Magharibi ‘A’ kubadilika na kujikita katika suala la kibiashara kwa kutafuta fedha na kuongeza Vizimba katika soko hilo ili kuleta ustawi wa biashara.

Aliiomba Benki ya CRDB kuendelea kushirikiana na Serikali na kuwakopesha fedha  wajasiriamali ili waweze kuendeleza biashara zao, huku akiahidi kuongezewa kiwango zaidi cha mitaji  vikundi vitakavyofanikiwa kurejesha mikopo ya awali.

Aidha, Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutembelea na kuona maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Maji katika eneo la Masingini (Masingini Scheme) unaojengwa na Mkandarasi kutoka Kampuni ya L&T Construction kwa gharama ya Dola Milioni 35.8, mradi unaohusisha ujenzi wa matangi mawili ya maji yenye uweezo wa ujazo wa Lita Milioni 18.

Akizungumza na wananchi wa maeneo ya mradi, Dk. Mwinyi alimpongeza Mkandarasi huyo kwa kuendelea na mradi huo vizuri na kuwataka watendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha miundombinu hiyo inaleta matumaini mema kwa wananchi juu ya upatikanaji wa huduma hiyo. 

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alipongeza mafanikio yaliofikiwa katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo katika Wilaya hiyo ya Magharibi ‘A’ , kupitia sekta za Maji, Afya, Elimu, Barabara pamoja na soko la Wajasiriamali na kusema anaridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, mbali na kasoro iliojitokeza kwa Mkandarasi anaejenga mradi wa Skuli ya Sekondari Mtopepo. 

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.