Habari za Punde

*Yasema Mfuko unatimiza malengo yaliyokusudiwa *Umeondoa hofu kwa wafanyakazi na kuongeza kujiamini *Watwaa Tuzo Maonesho ya Sabasaba 2022.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu (kulia) akipokea majarida na nembo ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kutoka kwa Meneja Mipango WCF,  Patrick Ngwila alipotembelea kwenye banda la Mfuko huo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, jana Julai 8, 2022.

NA KHALFAN SAID, SABASABA                                           

SERIKALI imesema inajivunia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa jinsi umeweza kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kuongeza matumaini kwa Wafanyakazi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi alipotembeela banda la WCF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyofikia kilele jana Julai 13, 2022.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambao ulianza kutekeleza majukumu yake miaka sita iliyopita, unatoa Fidia kwa mfanyakazi aliyeumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi kwa mujibu wa mkataba na mwajiri wake.

“Sisi kama Serikali tunaridhika sana na jinsi mnavyotekeleza majukumu yenu, mmewaondolea hofu wafanyakazi na sasa wanafanya kazi kwa kujiamini" alisema

Alisema na waajiri nao wamepata fursa ya kujielekeza katika biashara na uzalishaji mali kwani kazi ya kumuhudumia mfanyakazi anapopatwa na madhila yoyote akiwa kazini kama vile kuumia, kuugua na hata kufariki, WCF inachukua jukumu hilo.

"Tunaendelea kushuhudia, pamoja na kulipa fidia Mfuko pia unatoa huduma ya utengamao na kuwasaidia wale ambao wamepata maumivu kwenye viungo vyao wanapatiwa matibabu na wakati mwingine wanapopona wanarudi kazini na kuendelea na majukumu yao." Alifafanua.

Wakati huo huo Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeibuka mshindi wa tatu kati ya Wizara, Wakala na Taasisi zote za Serikali zilizoshiriki kwenye maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (Sabasaba 2022).

Ushindi huo umetangazwa wakati wa kilele cha Maonesho hayo Julai 13, 2022 ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isidory Mpango.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amewashukuru wadau wote waliotembelea Banda la WCF wakati wa maonesho hayo.

"Tunawashukuru sana viongozi wa Serikali pamoja na wadau wetu wote waliojitokeza kwa wingi sana mwaka huu kutembelea Banda la WCF. Kwa pamoja tumeshinda", amesema Dkt. Mduma.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (wapili kushoto), akipewa ufafanuazi kuhusu huduma za WCF na mmoja wa Maafisa wa Mfuko huo wakati alipotembelea banda hilo akiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. John Mduma (wapili kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Laura Kunenge.
Mhe. Katambi (kushoto) akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma alipotembeela banda la Mfuko huo.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi (wanne kushoto) akiwa na timu ya WCF ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. John Mduma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu (kulia) akipokea majarida na nembo ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kutoka kwa Meneja Mipango WCF,  Patrick Ngwila alipotembelea kwenye banda la Mfuko huo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, jana Julai 8, 2022.
Mkurugenzi Mkuu WCF akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mfuko huo huku akiwa ameshika tuzo hiyo.
Afisa Uhusiano Mwandamizi WCF, Bi. Sarah Reuben akionesha tuzo hiyo.
Shughuli za utoaji huduma kwa wadau zikiendelea

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.