Habari za Punde

Dk Mabodi asisitiza ujenzi wa Taifa

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,akizungumza katika Bonanza la michezo kwa ajili ya kuhamasisha zoezi la sensa na utamaduni wa wananchi kudai risiti za Elektroniki wakati wanaponunua bidhaa mbali nchini ili kuongeza mapato, lililofanyika uwanja wa Gombani ya Kale Pemba.
 

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, amewasisitiza Vijana kuendeleza utamaduni wa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika harakati za ujenzi wa Taifa.

Amesema utamaduni huo wa kujitolea  ndio kielelezo halisi cha uzalendo ulioasisiwa na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na wakakomboa nchi hadi ikapiga hatua kubwa za maendeleo zilizopo hivi sasa.

Hayo ameyaeleza wakati akizindua Bonanza la michezo kwa ajili ya kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu, lililofanyika katika kiwanja cha Gombani ya Kale Pemba.

Dk. Mabodi amewapongeza vijana,wadau,taasisi na wananchi kwa ujumla waliojitolea kufanikisha Bonanza hilo linalounga mkono juhudi za kimaendeleo zinazofanywa na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Alisema kwamba hafla hiyo imeandaliwa na vijana wazalendo kutoka Taasisi ya Nasimama na Dk.Mwinyi Foundation ambao wamekuwa ni mfano wa kuingwa katika harakati za kuunga mkono juhudi za Serikali.

“Zanzibar tuna historia kubwa katika masuala ya uzalendo wazee wetu walijitolea bila kujali maslahi binafsi na kuweka mbele maslahi ya nchi yaliyotuvusha na kujitawala wenyewe.

Hivyo bado vijana wa sasa licha ya kushiriki katika masuala ya michezo na fursa zingine bado haitoshi mnatakiwa mjitolee zaidi kwa nia ya kujijenga kiimani,utii,ukakamavu  na uzalendo uliotukuka.”, alisema Dk.Mabodi.

Alisema wananchi wanatakiwa kuunga mkono Chama cha siasa chenye sera na Ilani ya uchaguzi inayotafsiri maendeleo kwa vitendo na sio porojo na mbwembwe za kutafuta umaarufu usio na tija kwa umma.

Akizungumzia suala la sense alisema ni miongoni mwa sera zinazogusa maisha na mafanikio ya wananchi wote kwani wanapohesabiwa ndipo serikali inapata takwimu halisi za kuimarisha huduma za kijamii katika kipindi cha miaka kumi ijayo.

Amesema sense ya mwaka huu ni ya kisayansi kwani imebeba mambo mengi ambayo watu wa rika zote wakiwemo watu wenye ulemavu,makaazi,elimu na taarifa mbalimbali za kijamii yote yatazingatiwa.

Katika Bonanza hilo lililotanguliwa na zoezi la usafi katika hospitali ya Chakechake,matembezi ya kuhamasisha wananchi kushiriki sensa na matumizi ya risiti za Kielektroniki  michezo ya kuvuta kamba,ngoma za asili,mbio za kuku,kukimbia na gunia.

Wakati wa  jioni wamehitimisha na mchezo wa mpira wa miguu uliowakutanisha Timu za wakongwe wa Soka kisiwani humo ambao ni Timu ya Wete na Mkoani ambao wote wametoka sare kwa kufungana goli 1-1 na washindi wa michezo hiyo wamekabidhiwa zawadi mbalimbali zilizotolewa na waandaji wa bonanza hilo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.