Habari za Punde

Mhe Hemed ayafunga Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane leo


 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka Miundombinu ya kisasa katika Sekta ya Kilimo ili kukuza sekta hiyo Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Kauli hiyo wakati akifunga Maonesho ya Kilimo Nane Nane yanayofanyika  katika viwanja vya Dole Kizimbani wila ya Magharibi “A”.

Amesema  Serikali imetenga Jumla ya Shilingi Bilioni Sita (6.0) za Kitanzania kwa Mradi wa kurejesha urithi wa kijani ambapo Mradi huo utalenga kuendeleza uzalishaji Miche ya Miti ya Misitu na Matunda sambamba na Upandaji wa Miti katika Maeneo ya wazi ya Mashamba ya Serikali na Maeneo mengine mbali mbali.

Aidha ameeleza kuwa Fedha hizo pia zitahusika na Mradi wa kuendeleza Miundombinu ya Mifugo Maeneo mbali mbali, ununuzi wa Mtambo wa uzalishaji Gesi ya Niatrojeni kwa ajili ya kuhifadhia Mbegu za kupandishia Ng'ombe kwa Sindano.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali imekuwa Mstari wa mbele katika kujenga na kueneza Maendeleo Maeneo mbali mbali ikiwemo ujenzi wa Bababara zitakazosaidia kusafirisha mazao kwa urahisi.

"Nataka mtambue kwamba Serikali yenu imekuwa mstari wa mbele katika kujenga na kueneza maendeleo mbali mbali vijijini mwetu ikiwemo ujenzi wa Miundombinu ya Sekta zote za Kilimo, Barabara za ndani ambazo zitawasaidia Wakulima kuweza kusafirisha mazao yao kirahisi" Mhe. Hemed

Aidha ameeleza kuwa Mbali na ujenzi wa Miundombinu hiyo Serikali imejipanga kuwajengea uwezo juu ya Utumiaji wa Miundombinu ya umwagiliaji maji katika kukuza Uzalishaji wa mazao ya Kilimo  ikitambua asilimia kubwa ya Wananchi wanategemea Sekta hiyo.

"Serikali imekuwa ikifanya haya yote kwa kutambua Asilimia kubwa ya Wananchi wake wanategemea Sekta ya Kilimo kwa namna moja ama nyengine. Niwahakikishia juhudi hizi za Serikali zitaendelezwa ili tuweze kumtoa Mkulima pale alipo sasa kutoka Kilimo cha Kujikimu na kuwa Kilimo cha Biashara " Mhe. Hemed

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi imeipa kipaumbele Sekta ya Kilimo ili kuwasaidia Wananchi wake kujikimu kimaisha pamoja na kuwa na uhakika wa Chakula na lishe Bora.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Wizara Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa kuendelea kuandaa maonesho hayo na kueleza kuwa ni wajibu kwao kuendeleza Mashirikiano na juhudi ili Sekta ya Kilimo itoe matokeo yanayaotarajiwa katika Jamii.

Aidha amewaomba kuendelea kuyatumia Maonesho ya Nane Nane kuwa ni Jukwaa la kusambaza Teknolojia zinazoendana na wakati.

Kwa upande wake Waziri Wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili Na Mifugo Mhe. Shamata Shaame Khamis amesema kuwa wizara imejipanga kuhakikisha wanalizungunshia uzio eneo lote ambalo linafanyiwa maonesho hayo ili kulitunza na kuimarisha ulinzi ikiwa na maelekezo kutoka kwa Rais Wa Zanzibar Na Mwenyekiti Wa Baraza La Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi aliyoyatoa alipokuwa akiyafungua maonesho hayo.

Mhe.SHAMATA amesisitiza kuwa atahakikisha eneo la maoesho linatoa huduma bora kwa kila mtu anaefika katika maonesho hayo ili kuleta ufanisi nzuri kwa wananchi na amewata wadau mbali mbali kuzidi kuwaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya nane katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Pia Mhe. Shamata amemuhakikishia makamu wa pili kuwa wizara imejipanga kuleta wawekezaji kuja kwa wingi kuekeza hasa katika sekta ya ufugaji ili kuhakikisha zanzibari inajitegemea kwa kila kitu hasa katika chakula.

Nae Katibu Mkuu Wizara Ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili Na Mifugo Ndugu Seif Shaaban Mwinyi amesema kuwa katika maonesho hayo yalioanza tarehe 6/8/2022 wananchi wamepata fursa ya kujifunza mambo mbali mbali ya kilimo cha kisasa  na ufugaji wenye tija pia amesema kuwa lengo kuu la maonesho hayo ni kuwasaidia wananchi kupata elimu na kulima kilimo cha kisasa na chenyetija ya hali ya juu ili kuondokana na utegemezi wa chakula kutoka sehem nyengine.

Aidha Ndugu Shaaban amesema maoensho ya mwaka huu washiriki wameongezeka na kufikia 225 kupitia sekta mbali mbali za kiserikali na binafsi wakiwemo wajasiriamali ukilinganisha na miaka iliyopita pia wizara imejipanga kutumia Zaidi ya milioni MIA SITA  kwenye maonesho hayo.

Kauli mbiu ya mwaonesho ya mwaka huu “KILIMO NI BIASHARA SHIRIKI KUHESABIWA KWA MIPANGO BORA YA SEKTA YA KILIMO”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.