Habari za Punde

Waandishi wa Habari Wapata Mafunzo Kuhusiana na Saratani ya Tezi Dume

Baadhi ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkufunzi kutoka Kitengo cha maradhi yasioambukiza katika Hospitali ya rufaa Mnazi immoja Omar Abdalla Ali (hayupo pichani) kuhusiana na Saratani ya tenzi dume, juu ya athari zake na dalili zake, huko katika  Jumuiya ya Watu wanaoishi na Maradhi Yasioambukiza mpendae. 

Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar .19/08/2022.

Mratibu wa Kitengo cha Maradhi Yasioambukiza, katika  Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja, Omar Abdalla Ali ameitaka jamii kuweka utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuepukana na maradhi yasioambukiza .


Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi Yasioambukiza Mpendae, wakati akitoa mafunzo kwa Waandishi wa habari kuhusiana na Saratani ya tenzi dume .


Amesema  watu wanatakiwa kufanya mazoezi kabla ya kupata maradhi pamoja na kuwa na utamaduni wa kupima afya zao kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuepukana na maradhi yasioambukiza .


“Inashangaza sana  jamii yetu hatutaki kufanya mazowezi hadi mtu tayari keshapata kiharusi ndio anafanya mazowezi  tujitahidini kuufanya mwili utoke jasho na damu itembee vizuri “alisema Mratibu huyo.


Alifahamisha kuwa saratani ya tenzi dume(Prostate ) ni moja ya aina za kawaida za saratani kwa wanaume ambayo inakuwa pole pole na inakabiliwa na kinga ya (Prostate  ) ambapo inaweza kusababisha madhara makubwa ambayo huweza kuonyesha ishara au isiwe na ishara yoyote  .


Aidha alisema saratani ya tenzi dume mara nyingi huwapata watu wazima wenye umri wa miaka 45 na kuendelea na dalili zake ni kupata maumivu wakati wa haja ndogo kuziba kwa mkojo pamoja na uwezo hafifu wa kurusha mkojo wakati wa haja ndogo .


Alieleza kutoka damu kwenye mkojo na kushindwa kumaliza mkojo ni ishara ya kuwa tenzi dume imeathirika lakini udhaifu katika utoaji wa mkojo inawezekana kutokea kwa kuvima tenzi dume bila ya kuwa na sarataniya tenzi dume.


Mratibu huyo alieleza kuwa vichocheo vya maradhi haya ni unene uliokithiri,ulaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta,mfumo mbaya wa ulaji, maambukizi ya mara kwa mara kwenye tenzi dume pamoja na ukosefu wa mazoezi .


Nae Meneja wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi  yasioambukiza  Haji Khamis Fundi ameitaka jamii kuchunguza afya zao mara kwa mara kwani kufanya hivyo kutasaidia kujiweka katika hali ya usalama kiafya .


Alifahamisha kuwa iwapo  mtu atagundulika na  tatizo la maradhi ya  saratani ya tenzi dume katika hatua za awali atapatiwa tiba na kupona kwa haraka iwapo saratani hiyo ikiwa ishaathiri  uwezekano wa kupona huwa ni mdogo na matibabu yake huwa na gharama kubwa .


Akitoa wito kwa jamii kutopuuza maagizo na ushauri wa wataalamu wa afya kwa kuchunguza afya na kufanya mazowezi kabla ya kuumwa ,na  kuwataka wanaume wasiwe na wasiwasi wa kuchunguzwa saratani ya tenzi dume kwani kuna aina nyingi za uchunguzi  wa maradhi hayo .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.