Habari za Punde

Walimu watakiwa kuwajibika na kuimarisha nidhamu

Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari,Msingi na Maandalizi za SMZ na Binafsi Mkoa wa Kaskazini Pemba  wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ( hayupo pichani) kwenye kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa baraza la wawakilishi Wete
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari,Msingi na Maandalizi za SMZ na Binafsi Mkoa wa Kaskazini Pemba katika ukumbi wa mikutano Baraza la Wawakilishi Wete.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari,Msingi na Maandalizi za SMZ na Binafsi Mkoa wa Kaskazini Pemba katika ukumbi wa mikutano Baraza la Wawakilishi Wete.


Na Ally Mohammed , OMPR

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka walimu wakuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kuwajibika ipasavyo ili kuleta ufanisi katika  kazi.

Mhe. Hemed ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na walimu wakuu wa skuli za Maandalizi, Msingi na Sekondari za Serikali na Binafsi Kwa Mkoa wa kaskazini Pemba kwenye kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa baraza la wawakilishi wete.

Ameeleza kuwa walimu Wakuu ndio wasimamizi wakubwa kwenye Sekta ya Elimu hivyo amewataka kuimarisha Nidhamu, Uwajibikaji na kumtaka kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa maslahi ya Taifa.

"Suala la nidhamu naomba walimu wakuu acheni muhali kuna walimu hawaji kazini kwa wakati, watoro, hawana muongozo katika kufundisha hili lifatilieni kwa nguvu zote ili tuweze kupata wataalamu na viongozi bora hapo baadae” Amesema

Mhe. Hemed ameeleza kuwa ni vyema kila mwalimu mkuu kuhakikisha anatoa muongozo kwa walimu waliopo chini yake ili kujua maslahi yake na kuweza kuwapatia haki zao na kuimarisha utawala bora.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha inawalipa walimu wote wanaodai stahiki zao ili waweze kufanya kazi kwa weledi  na kutoa wataalamu bora hapo baadae.

Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dkt. Hussen Ali Mwinyi itahakikisha inawalipa walimu wote stahiki zao ikiwemo pesa za likizo hata waliokuwa kwenye ugatuzi.

“kila anaestahiki kupata stahiki yake serikali ya awamu ya nane itahakikisha analipwa kupitia utaratibu uliowekwa na Serikali ili kuweza kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuhakikisha wanapatikana wataalamu na viongozi bora wa hapo baadae” amesema.

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka uongozi wa wizara hio kuhakikisha ajira ambazo zimetangazwa na Serikali zifate utaratibu ambao utasaidia kuwapata walimu ambao wanasifa stahiki.

Pia ameitaka wizara kuhakikisha kila mwalimu ambae atakaeajiriwa kufanya kazi katika sehemu husika ni vyema uongozi kusimamia mfanyakazi huyo anafanya kazi sehemu ambayo ameomba kuifanyia kazi.

Mhe. Hemed ameiagiza wizara kuhakikisha nyumba ambazo zimejengwa kwa ajili ya walimu waweze kupatiwa walimu husika na sio kukaa mtu yeyote ambae hahusiki kuishi eneo hilo.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. LEILA MOHAMED MUSSA amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha na kuboresha skuli zote ambazo zinataka kufanyiwa ukarabati kupitia pesa za UVIKO 19.

Mhe Leila wizara itahakikisha inachukua hatua stahiki kwa walimu wote wa skuli za Serikali na binafsi ili kuhakikisha Serikali inayafikia malengo ambayo imejiwekea kwa wananchi wake.

Kwa upande wao walimu wakuu wa skuli za Mkoa wa Kaskazini Pemba wameiomba Serikali kuondosha changamoto zote zinazowakabili walimu wa mkoa huo ikiwemo uchakavu wa majengo, uhaba wa walimu, vitendea kazi pamoja na stahiki zao ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa Maslahi ya Taifa.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais amekutana na madaktari na wauguzi wa mkoa wa kaskazini Pemba kwenye ukumbi wa Jamuhuri Wete na kuwataka kuongeza uwajibikaji ili kuokoa maisha ya wazanzibari.

Mhe. Hemed amewahakikishia madaktari hao kulipwa kila mtu anachostaki kwa kuzingatia sheria za utumishi na Serikali itahakikisha kila mtu atalipwa fedha zake zote zikiwemo na eria zao.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais amemuagiza kaimu Afisa Mdhamini Wizara ya afya Pemba kufatilia posho la muda wa ziada kwa madaktari wa mkoa wa Kaskazini ili kila mmoja apate haki yake.

Mhe. Hemed amewataka wataalamu hao kuweza kutumia  lugha nzuri kwa wagonjwa wanaofika hospitalini ili kuweza kupata faraja na Serikali imejipanga kutatua changamoto zote zinazoikabili sekta ya Afya ikiwemo upatikanaji wa vifaa kinga na Tiba.

Amesema Serikali imeamua kujenga hospitali kubwa za kisasa kila Wilaya na Mikoa  ili kuweza kutoa huduma bora za Afya kwa wananchi wake.

Kwa upande wake waziri wa Afya Mhe.Nassor Ahmed Mazurui amesema kuwa Wizara imejipanga kupeleka wafanyakazi kwenda kusoma hasa kwenye kada ya mionzi ndani ya mwaka huu.

Mhe.Mazurui amesema kuwa Serikali imeamua kubinafsisha baadhi ya huduma ikiwemo za maabara ili kuboresha huduma hio na kuwataka madaktari kila mmoja kuweza kutimiza wajibu wake ili kuokoa maisha ya wazanzibari na watanzania kwa ujumla.

Nao madaktari wa mkoa huo wameiomba Serikali kuwaboreshea maslahi yao na kuweka vifaa kinga na tiba ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.