Habari za Punde

Umuhimu wa Jamii Kujikita katika kufanya mazoezi kwa kigezo kuwa hujenga afya, kuleta urafiki, upendo na kushajiisha amani.

 

MKE wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation Mama Mariam Mwinyi akijumuika na Wanamichezo wa vikundi mbalimbali vya Wilaya ya Magharibi “A” Unguja katika matembelezi ya Kilomita 5.5 yaliyoazia katika eneo la regeza mwendo na kumalizikia katika viwanja vya mpira Dole kwa mazoezi ya pamoja ya viungo yaliyofanyika leo 24-9-2022.

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariam Mwinyi amesisitiza umuhimu wa jamii kujikita katika kufanya mazoezi kwa kigezo kuwa hujenga afya, kuleta urafiki, upendo na kushajiisha amani.

Mama Mariamu amesema hayo huko Dole Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja baada ya kukamilisha mazoezi ya viungo, yaliowashirikisha wanamichezo kutoka makundi  mbali mbali, ambapo yalitanguliwa na matembezi ya hiari yalioanzia Halmashauri ya Wilaya Magharibi ‘A’ Kianga  hadi Viwanja vya Dole.

Akizungumza na wanamichezo hao amesema mazoezi huleta afya na kufafanua kuwa watu wenye afya huwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi, hivyo akatoa wito kwa jamii kufanya mazoezi kila inapopatikana nafasi; na kulifanya jambo hilo kuwa sehemu ya maisha yao.

Alisema kupitia mikusanyiko ya aina hiyo jamii hupata fursa ya kupokea taarifa mbali mbali , ikiwemo changamoto zinazowakabili kwa dhamira ya kuzitafutia ufumbuzi.

Mama Mariamu alitumia fursa hiyo kuikumbusha jamii  juu ya umuhimu wa kuchanja katika kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, akibainisha namna watu kadhaa walivyopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Aidha, alielezea umuhimu wa wazazi na walezi katika kusimamia maendeleo ya elimu ya watoto wao pamoja na kufuatilia nyendo zao kwa kigezo kuwa kumekuwa na baadhi ya wanafunzi wanaotoka nyumbani na kuishia njiani wakati wakielekea skuli kwa sababu mbali mbali za utoro.

“Elimu humpa mtu taarifa , maarifa na ustadi pamoja na kusimamia maadili..........elimu ni ufunguo uanaofungua fursa mbambali za kimaisha”, alisema.

Alieleza kuwa Taifa linahitaji wataalamu katika fani mbali mbali, na kusema  elimu ni muhimu katika kufikia malengo hayo.

Nae, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema Wizara hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Mama Mariamu Mwinyi kupitia Jumuiya yake ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) katika kuihamasisha jamii  kufanya mazoezi.

Mapema, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa  Kitwana Mustafa aliwashukuru wanamichezo wote walioshiriki mazoezi hayo, ambapo pamoja na amambo mengine  alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kijamii zinazokabili Wilaya hiyo, akitolea mfano wa suala la utoro maskulini.

Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo Suzan Kunambi, aliwashukuru wananchi kwa kuitikia wito wa kushirki katika mazoezi hayo, ikiwa ni hatua ya  kuunga mkono ZMBF na kusisitiza azma ya Ungozi wa Wilaya hiyo  kuendeleea kuwashajiisha. 

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.