Habari za Punde

CHAVIZA yafanya uchaguzi wa viongozi

 Na Rahima Mohamed   Maelezo  31/10/2022

 

Mkurugenzi wa Baraza la watu wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe  amewataka viongozi wa chama Cha Viziwi, kuhakikisha wanatoa mafunzo ya lugha ya alama kwa Viziwi na Jamii Ili kurahisisha Mawasiliano baina yao. 

 

Debe alitoa wito huo wakati akifungua mkutano mkuu wa Uchaguzi  chama cha Viziwi Zanzibar ( CHAVIZA) huko katika skuli ya Sekondari ya Dkt Ali Mohamed Shein Rahaleo Mjini Unguja. 

 

Amesema   watu wenye ulemavu wa uziwi wanakabiliwa na changamoto za kuwasiliana hivyo mafunzo yatakayotolewa yatarahisisha   upatikanaji wa mahitaji yao ya kila siku.

 

Aidha amesema ni  jukumu la viongozi hao kuhakikisha   wanandaa mikakati madhubuti  ambayo itawezesha upitikanaji wa mafunzo hayo ili jamii iwe na uelewa zaidi juu ya watu wenye ulemavu wa uziwi. 

 

"Lengo la serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwahudumia wananchi wote ikiwemo  watu wenye ulemavu nao wananufaika na fursa mbalimbali  za kimaendeleo zinazotolewa na serikali yao" Amesema Mkurugenzi huyo.

 

Aidha amesema mabadiliko ya katiba ni jambo muhimu kwa sababu ndiyo maazimio ya wanachama na kuwataka viongozi wapya wajitahidi kukiendeleza Chama hicho kuhakikisha watu wenye ulemavu wa uziwi wanatambulika na kutetea haki za wanachama hao.

 

Mkurugenzi huyo amekipongeza Chama hicho kwa  kukamilisha mchakato huo kwa kukutana kufanya mkutano mkuu ambao unatoa maamuzi makubwa katika jumuiya zao kutokana na jumuiya nyingi kushindwa kufikia hatua hiyo.

 

Akisoma ripoti ya Utekekelezaji Afua Nassour Hassan amesema Chaviza kimependekeza Wizara ya elimu itengeneze muongozo wa kufundishia lugha ya alama na jamii iendelee kuhamasishwa kujiendeleza kivitendo katika kujifunza lugha hiyo na kuifanyia kazi ipasavyo.

 

Aidha amelitaka Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu kushirikiana bega kwa bega na CHAVIZA pamoja na kuongeza wafanyakazi wa muda ili kurahisisha  upatikanaji wa huduma endelevu kwa wanaofika ofisini hapo.

 

Nao Mwenyekiti na wajumbe wa Chama cha viziwi Zanzibar Taifa wamesema watahakikisha wananaleta maendeleo katika jumuiya yao pamoja na kuhakikisha viziwi wanafaidika na haki zote za kibinadamu kwa kiwango cha juu pamoja na kutatua changamoto wanazokumbana nazo katika harakati zao za kila siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.