Habari za Punde

Mikutano ya Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika huwaunganisha wajumbe - Dk Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema mikutano  ya Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika ni majukwaa muhimu katika kuwaunganisha wajumbe na kupata fursa ya kujadili masuala muhimu ya kisheria.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika Ufunguzi wa Mkutano wa sita wa Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika, uliofanyika Hoteli ya Madinat Al Bahr , ilioko Mbeni Mkoa Mjini Magharibi.   katika kleta amslahi mapana na ufanisi katika shughuli zinazofanywa na Mabunge hayo.

Amesema katika kuleta ufansi na maslahi mapana katika shughuli zinazofanywa na Mabunge, kuna mambo mengi yanayowaunganisha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika, ikiwemo suala la mila na tamaduni za Kiafrika, hivyo mikutano hiyo hujenga uhalali wa kuwa na taasisi ya pamoja.

Aliwataka washiriki kulitumia vyema jukwa hilo katika kujifunza na kubadilishana uzoefu miongoni mwao, badala ya kutegemea uzoefu kutoka nchi za Kimagharibi.

“Pamoja na hatua kubwa za kimaendeleo walizofikia, ni wazi yapo mambo mengi kwao yasioendana na mazingira yetu, zikiwemo mila na tamaduni zetu”, alisema.

Alisema mkutano huo ni muhimu sana kwa Mabunge na Serikali katika nchi za Kiafrika, kwa kuzingatia kuwa Wanasheria hao wanahusika moja kwa moja na utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na Mabunge, ikiwemo suala la utungaji wa sheria.

Aidha, aliwataka wajumbe hao kutumia nafasi zao kushauri mambo watakayohisi ni muhimu katika kukiimarisha chama hicho.

Dk. Mwinyi alisema Mabunge mengi Barani Afrika kama ilivyo kwa Mabunge mengine Duniani hujumuisha wabunge wenye mitazamo tofauti ya kisiasa, hivyo akatanabahisha  wajibu walionao katika kuitambua hali hiyo na kuiheshimu katika utendaji wa majukumu yao.

“Mnapaswa kutoa ushauri kwa wateja wenu wote kwa misingi ya usawa bila ya kusukumwa na itikadi za kisiasa, mfanye kazi kwa kuzingatia utaalamu mlionao kwa misingi ya taaluma zenu na kuweka mbele maslahi ya umma na ustawi wa Bara la Afrika”, alisema.

Rais  Dk. Mwinyi alibainisha furaha aliyonayo  kutokana na jukwaa hilo kusheheni wanasheria wa Afrika, likiakisi mikakati ya Umoja wa Afrika, ikiwemo Agenda ya 2063, inayosisitiza Umoja miongoni  mwa nchi za Afrika.

Alisema ni jambo jema kwa  Chama hicho kuwa na Kanuni za Nairobi “Nairobi Principles” kwa mantiki ya kuwa zimezingatia umuhimu wa kuwajengea wanasheria wa Mabunge ya Afrika weledi, ushirikiano, umoja na kuimarisha utendaji.

Aidha, alisiitiza umuhimu wa kuzitumia kanuni hizo ili kupata matokeo mazuri yatakayoweza kuyasaidia Mabunge na Serikali katika Bara hilo la Afrika.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alilipongeza Bunge la Afrika (Pan African Parliment) kwa kuunga mkono juhudi za wanasheria wa Mabunge ya Afrika, ambapo kimsingi yanasimamia Ajenda ya Umoja wa Afrika, yenye azma  ya kuwaunganisha Waafrika.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wajumbe kutembelea maneo ya Vivutio vya Utalii hapa Zanzibar na kuwa Mabalozi wa kuwasimulia wengine pale watakaporejea nyumbani, akibainisha  Zanzibar kuwa na vivutio vingi vya Utalii, ikihusisha maeneo ya Kihistoria, utamaduni, fukwe, wanyama pamoja na mazingira yenye kuvutia.

Nae, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali Maulid  alisema kuna umuhimu kwa kujenga utamaduni kwa Wanasheria wa Mabunge ya Afrika kutembeleana, huku akabainisha uwepo wa fursa kwa wajumbe wa Mabunge hayo kuja nchini kujifunza katika Baraza la Wawakilishi.

Alisema Baraza la Wawakilishi lipo tayari kuendeleza ushirikiano na Mabunge ya Afrika pamoja na kusaidia harakati za Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya  Afrika kwa mustakbali wa maendeleo ya chama hicho.

Spika Maulid Alisema Mabaraza ya Wawakilishi pamoja na Mabunge yamekuwa yakitegemea sana mchango wa wanasheria,  hivyo akabainisha imani yake kuwa mkutano huo utatumika kuwajengea uwezo wanasheria hao, kupata uzoefu pamoja na kujiamini.

Mapema, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Mabunge Afrika Mussa Kombo Bakar alisema Kongamano hilo la  Sita wa Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika limezishirikisha wajumbe kutoka nchi mbali mbali za Afrika, ikiwemo Tanzania, Zanzibar ,Kenya, Uganda, Ghana, Libya, Nigeria, Afrika Kusini pamoja na Msumbiji.

Alizitaja nchi nyingine kuwa ni pamoja  Syshelles, Sierra Leone, Eswatini, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Mabunge ya Kikanda ECOWAS, EALA pamoja na Provinces za  Kenya na Afrika Kusini.

Katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alipata fursa ya kuzindua Jarida na Tovuti ya Chama cha Wanasheria wa Mabunge Afrika pamoja na Kukabidhi Cheti cha Usajili wa Chama hicho.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.