Habari za Punde

Jamii, kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuhakikisha wanawafichua wanaotenda vitendo hivyo na kuchukuliwa hatua.

Na Maulid Yussuf WMJJWW Zanzibar 

Ikiwa katika siku 16 za wanaharakati wa kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia nchini,  Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa ushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutoa  elimu juu ya matukio hayo wa lengo la kutokomeza vitendo hivyo nchini.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, bwana Mohamed Jabir Makame ameiomba jamii, kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuhakikisha wanawafichua wanaotenda vitendo hivyo na kuchukuliwa hatua.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo juu ya kizazi chenye usawa ili kuweza kuandaa mikakati itakayosaidia kupunguza ukatili na udhalilishaji wa kijinsia nchini,  katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,  Maisara Mjini Unguja  amesema hatua hiyo itasaidia katika kubadilishana mawazo na kutathmini katika mapambano ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia. 

Amesema kuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia 
Wazee na Watoto inaendelea na jitihada za mapambano dhidi ya matendo hayo ili kuhakikisha yanamalizika kabisa nchini.

Amesema ni matarajio ya Wizara ni kuwa baada ya mafunzo hayo ya siku mbili ni kuona vile vichocheo vilivyojitokeza vitachangia kupanga mikakati katika Taasisi zao au Jumuiya zao kupanga mikakati ya kusaidia mapambano dhidi ya ukatili na udhalilishaji nchini.

"Matarajio yetu baada ya siku hizi mbili zitasaidia kuiwezesha jamii na hadhira katika kuifanyia kazi katika mapambano"amesisitiza Kaimu Mkurugenzi  huyo.

Nae Afisa wa Programu za jinsia kutoka Shirika la Idadi ya Watu Duniani UNFPA, bwana Ali Haji Hamad  amesema kua lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwasaidia  jamii kuweza kuzungumza katika mapambano ya ukatili wa udhalilishaji nchini.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa Masuala ya jinsia bwana Iddi Rajabu Mzirai amesisitiza uwepo wa usawa wa jinsia kwa jamii ili kuiwezesha jinsia ya kike kupata nafasi ya kushiriki katika masuala mbalimbali ya uongozi pamoja na kutoa maamuzi.

Aidha amesema kuwa hivi sasa kumeibuka wimbi la ulawiti wa watoto wa kiume hali ambayo inapelekea Taifa kuwa katika hali mbaya kwa watoto wa kiume.

Pia amesema kutokana na tamaduni za kizanzibari juu ya mtoto wa kike kupata ujauzito,  kumepelekea kuwepo tatizo la utoaji ovyo wa mimba kwa watoto hali ambayo ni hatari kutokana na afya zao.

Hivyo amewataka jamii kuamka na kushirikiana katika kuwalea na kuwalinda watoto ili kuwaepusha na vitendo mbalimbali vya Ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.