Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo wakati akisoma Hotuba ya kuakhirisha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Kumi la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Amesema upatikanaji wa huduma ya Maji safi na Salama kwa Zanzibar umefikia asilimia Sitini na Sita hali ambayo inaonesha namna Serikali ya Awamu ya Nane ilivyokita kuwapatia huduma hiyo wananchi wake.
Ametumia Fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuitunza miundombinu ya Maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwafaa wananchi wengi.
"Nachukua nafasi hii kutoa wito kwa Wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuitunza na kuienzi miundombinu inayopita katika Maeneo yao wanayoishi ikiwemo miundombinu ya Maji"
Akigusia Sekta ya Afya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali imeridhika na ujenzi wa Hospitali za Wilaya na Mkoa kwa iliyofikia na Kuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya kuendelea kuwasimamia Wakandarasi ili kuweza kukamilisha Ujenzi huo kwa wakati.
Aidha ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuweka vifaa vya kisasa pamoja na kuhakikisha Hospitali zote zina Madaktari Bingwa na wataalamu wote wa Afya wanaohitajika katika kuwapatia huduma bora Wananchi wake.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema Serikali imepunguza gharama za uungwaji wa Umeme kwa wananchi wake ili waishi maisha bora kwa kufurahia huduma hiyo.
Aidha amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mtumishi atakaekwenda kinyume na Sheria za utumishi na kuwataka wananchi kutojihusisha na Masuala ya uvujaji wa Mapato wa Shirika la umeme ikiwemo kuchezea Mita kwa kuiba Umeme.
Pamoja na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewasisitiza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa mstari wa mbele kusimamia ukusanyaji wa Mapato na kuwataka wananchi kushirikiana na Mamlaka husika kusaidia Suala la ukusanyaji wa mapato.
Aidha ameushukuru Uongozi wa Mamlaka ya kuzuwia Rushwa na uhujumu wa uchumi Zanzibar (ZAECA) kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia udhibiti wa Mapato na kuzuwia rushwa na uhujumu wa uchumi.
Vile vile, ametumia fursa hiyo kuwasihi Watumishi wa Umma kuacha mambo yote yanayoashiria masuala ya rushwa, Wizi na urasimu na badala yake wafanye kazi kwa uadilifu.
Pia Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeahidi kufanya Mapinduzi makubwa katika miundombinu ya Bandari, Barabara na Viwanja vya Ndege na kuwaomba Wananchi kuendelea kutoa mashirikiano makubwa kwa Serikali ili kuwesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza uwepo wa Utawala Bora na Nidhamu ili kusaidia kuleta Maendeleo endelevu kwa Maslahi ya Wazanzibari
Kikao cha Baraza la Wawakilishi kimeakhirishwa hadi siku ya Jumatano tarehe 15 Februari, 2023
No comments:
Post a Comment