Habari za Punde

Tamko la Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Yampongeza Dkt.Ali Mohamed Shein,Makamu Mwenyekiti wa CCM - Zanzibar Mwaka 2012 – 2022

Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, katika Kikao chake kilichofanyika Dodoma, tarehe 06 Disemba 2022, pamoja na mambo mengine, ilifanya tathmini ya Mwenendo wa Uongozi wa Chama katika kipindi cha miaka mitano (2017 – 2022).

Katika kikao hicho, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imempongeza Dkt. Ali Mohamed Shein (Makamu Mwenyekiti wa CCM – Zanzibar) pamoja na viongozi wote wa Chama wa ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya, Majimbo, Kata/Wadi na Matawi kwa uongozi wao uliotukuka na heshima kubwa waliokipatia Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi chote cha miaka mitano (2017 – 2022).

Kipekee, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake mahiri wenye kuzingatia weledi, uadilifu, uzalendo, busara na hekima kwa nyadhifa zote alizotumikia katika Chama na Serikali zote mbili; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hakika, aina ya uongozi alioonesha Dkt. Ali Mohamed Shein ni Dira na Mwongozo kwa ustawi wa Chama chetu na Maendeleo ya Taifa letu. Kwa uchache, kutokana na uongozi wake, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, itakumbuka misingi imara ifuatayo iliyowekwa na Dkt, Ali Mohamed Shein wakati anaponga’atuka katika uongozi wa Chama: -

(a)     Uboreshaji wa Miundombinu ya barabara, madaraja, uwanja wa ndege wa Kimataifa, huduma za Elimu, Afya na Maji. Mfano, ujenzi wa barabara ya Kaskazini Unguja kuanzia Bubu hadi Kinyasini na barabara katika Mikoa miwili ya Pemba, pamoja ujenzi wa Skuli za ghorofa katika Wilaya zote 10 za Zanzibar.

(b)     Uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa umma. Mfano, Kuongezeka kwa kima cha chini cha Mishahara hadi shilingi 300,000/= kwa mwezi sambamba na kuanzisha pensheni ya wazee kwa kuwapatia kima cha shilingi 20,000/= kwa mwezi kila mzee mwenye umri wa miaka 70.

(c)      Dkt. Ali Mohamed Shein alisimamia maridhiano ya kisiasa kwa kuasisi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa.

(d)     Dkt. Ali Mohamed Shein alisimamia harakati zilizowezesha kupatikana kwa ushindi wa CCM wa kihistoria wa asilimia 76 katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Katika uchaguzi huo, CCM iliweka historia ya kushinda majimbo 14 kati ya 18 kwa upande wa Pemba, jambo ambalo halikuwahi kutokea tangu kuasisiwa kwa siasa za Mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

(e)      Kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wa CCM na Jumuiya zake katika ngazi zote za uongozi kuanzia Shina hadi Taifa.

Kwa kuhitimisha, Chama cha Mapinduzi, kinamshukuru Dkt. Ali Mohamed Shein kwa mchango wake alioutoa kwa Chama na Serikali akiwa Kiongozi. Aidha, Chama kitaendelea kutumia uzoefu wake wa uongozi katika ushauri wa masuala mbalimbali. Mwisho, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa inamtakia siha njema katika majukumu yake.

 

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.