Na Khadija Khamis -Maelezo Zanzibar,27/01/2023.
Katibu wa Kikosi Kazi cha Utekelezaji wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar(ZACCEP,) ambae pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatibu Makame amewataka watendaji kutekeleza majukumu yao kiufanisi ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Hayo ameyaeleza huko Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Maruhubi alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kikao kazi cha Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya miezi mitatu Oktoba hadi Disemba 2022..
Amesema kila Mjumbe anaewakilisha Taasisi yake iliyomo kwenye mpango huo ni vyema kusimamia utekelezaji wa majukumu na kuwasilisha ripoti ili kuonyesha maendeleo na changamoto zilizopo .
Alifahamisha kuwa iwapo wajumbe hao watafanyakazi kwa mashirikiano na bidii kutasaidia kufikia malengo yaliyotarajiwa kuliko kufanyakazi Kwa mazowea,
Alieleza kuwa bado kumekuwa na mazingira machafu Katika baadhi ya maeneo mbali mbali ya Zanzibar jambo ambalo ni hatarishi kwa kusababisha mripuko wa maradhi ya kipindupindu.hivyo aliagiza Taasisi husika kuchukuwa hatua stahiki kusimamia
"Kwani hatuwezi kudhibiti taka ikawa mfano kama Arusha na Moshi isiwe kila siku sisi tunakwenda kujifunza kwao ," Alisema Katibu huyo.
Nae Mratibu wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar Makame Ame Simai ameeleza changamoto mbali mbali zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa Mpango wa kipindi cha Mwaka mmoja uliopita ambao ulitekelezwa na Taasisi mbali mbali zilizomo katika mpango .
Aidha alisema changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huo ni kukauka kwa visima 32 vilivyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa kiangazi pamoja na kukosekana kwa gari ya kusafirishia maji taka hasa kwa upande wa Pemba na sehemu husika ya kumwagia maji hayo.
Nae Mjumbe kutoka Manispaa ya Magharibi ‘B’ Yussuf Mati Ali amesema wameondoa majaa mbali mbali ambayo sio rasmi katika maeneo ya kivigo Mwanakwerekwe, Taveta, ,Magirisi pamoja na Magereza na kusafisha mitaro ya kombeni, mazizini na mwanakwerekwe.
Vile vile alisema wamefanya ukaguzi kwa wafanyabiashara wa mikahawa 83 na mamalishe 50 kwa upande wa wilaya ya magharibi ‘B’ na baadhi walifungiwa na wengine kutoleshwa faini ya papo kwa papo.
Kwa upande wa wajumbe wametoa ushauri wa kuongezawa mjumbe kutoka shirika la umeme ili kuongeza nguvu katika uendeshaji wa visima vya maji kutokana na upungufu wa umeme hasa unapokuwa mdogo husababisha kuunguza mashine pamoja na kushindwa kusambaza maji katika maeneo mbali mbali .
No comments:
Post a Comment