Mkufunzi Ramadhan Khamis Ramadhan akitoa mada kwa Vijana waliofika katika ufunguzi wa mafunzo ya Uongozi na usimamizi wa fedha, huko ukumbi wa Skuli ya John Magufuli Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi “B” Januari 26,2023.
Picha na Miza Othman BTMZ.
Na Khadija Khamis – Maelezo , 26.01.2023.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khamis Abdalla Khamis amewataka vijana kuanzisha miradi yenye kuleta tija ili kujiajiri.
Aliyasema hayo katika Ukumbi wa Skuli ya John Magufuli Mwanakwerekwe,Wilaya ya Magharibi 'B'
wakati wa Mafunzo ya Mabaraza ya Vijana kwa Wilaya saba za Unguja .
Amesema iko haja kwa vijana kuandaa miradi mbalimbali na kuisimamia kwa uaminifu na uandilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuleta tija na kufikia malengo waliyokusudia
Aidha alifahamisha kuwa Mafunzo yanayotolewa Kwa vijana hao ni Uongozi na usimamizi wa Fedha ,Utalii na Uwandishi wa Miradi Usimamizi na Uendeshaji wa Miraadi ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 hadi 2025 Ibara ya 210 (C).
Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Salim Issa Ameir amewafahamisha vijana kuwa wabunifu kwa kuandaa miradi kulingana na mahitaji ya sehemu husika ili kuleta mafanikio na kupata soko .
Alisisitiza kwamba pindi vijana wakipatiwa Fedha za miradi kuwa wazalendo Kwa kuzisimamia na kutoa ripoti za uingiaji na utokaji wa fedha hizo ili kuleta maendeleo ya utekelezaji pamoja na kubainisha changamoto zinazojitokeza
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni (BASSFU) Dkt.Omar Abdalla Adam amewasisitiza Vijana kuwa makini katika kuisimamia raslimali Fedha za miradi ambazo zinazotoka serikalini na wafadhili ili kuleta tija na kuzifikia ndoto walijiwekea.
Kwa upande wa Afisa Mipango Muandamizi Ramadhan Khamis Ramadhan akitoa mada kuhusiana na namna ya kuandaa miradi na njia bora za utekelezaji wa miradi hiyo.
Alifahamisha jinsi ya kuratibu na kuisimamia pamoja na kujipangia malengo ya baadae ya miradi ili kuleta maendelo na kufikia matarajio
Mafunzo ni ya siku moja yaliyowashirikisha zaidi ya Vijana 200 wa Wilaya saba za Unguja ambayo yameandaliwa na Baraza la Vijana Zanzibar.
No comments:
Post a Comment