Na Khadija Khamis –Maelezo, Zanzibar.11/01/2023.
Maonyesho ya Kitaifa ya Utalii na Uwekezaji , (Zanzibar Tourism Investment and Travel Exhibition –ZTITE ) yanatarajiwa kuanza - Tarehe 9 Hadi 11 Februari katika Makumbusho ya Amani na ya Viumbe hai hapo Mnazimmoja
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Hafsa Mbamba wakati akizungumza na waandishi wa habari huko katika Hoteli ya Emerson in Space Mji Mkongwe.
Amesema maonyesho hayo ni ya mara ya mwanzo kufanyika hapa Zanzibar ambayo yanatarajiwa kupokea wageni 200 kutoka nchi mbali mbali .
Amesema lengo la kufanyika maonyesho hayo katika eneo la makumbusho ni kuifanya Sekta ya Utalii kwenda sambamba na Mambo ya Kale kwa kuleta maendeleo ya taifa na urithi wa vizazi vinavyo.
Aidha amesema kufanyika kwa Tamasha hilo ambalo litasimamiwa na kamisheni ya utalii kutasaidia kutangaza maeneo ya kihistoria kitaifa na kimataifa ili wageni wengi wapate fursa ya kutembelea maeneo hayo pamoja na kukuza mapato ya Taasisi na Serikali kiujumla.
Alifahamisha kuwa Zanzibar ina maeneo zaidi ya 86 ambayo yameainishwa na kutangazwa kupitia gazeti la Serikali hivyo ni fursa pekee ya kutangazwa maeneo hayo kupitia maonyesho.
Katibu huyo alisema kuwa kufanyika kwa maonyesho hayo yatasaidia kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana Zanzibar jambo ambalo litaimarisha sekta ya utalii na sekta mbali mbali.
Alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwakaribisha wawekezaji katika sekta mbali mbali ikiwemo Utalii,Kilimo,Makaazi Afya na nyenginezo kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya Zanzibar.
Hata hivyo amesema Serikali imekusudia kuongeza idadi ya Matamasha au maonyesho jambo ambalo litasaidia kuitangaza Zanzibar kuifanya kuwa maarufu zaidi kitaifa na kimataifa na kueweka vyema kiutalii katika ramani ya dunia hasa katika nchi za Falme za Kiarabu na Asia .
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Mariamu Mohamed Mansab amesema maonyesho hayo yanayotarajiwa kufanyika katika makumbusho yatakuwa ya kimataifa na kibiashara zaidi tofauti na maonyesho mengine hayo yatakuwa na utaratibu maalum ya kuingia ili kutoa fursa nzuri kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi .
Amesema kutakuwa na kujisajili kwa washiriki wa maonyesho hayo ambao washiriki watajisajili kwa njia ya mtandao na kutakuwepo na viingilio katika maonyesho hayo .
Alieleza kuwa kuwapatia wageni fursa ya kutembelea katika sehemu za vivutio kutasaidia kujitangaza wakati watakaporudi katika nchi zao watakuwa mabalozi wa kuitangaza Zanzibar.
No comments:
Post a Comment